Mama mjamzito mkazi wa Kijiji cha Kidubwa wilayani Mkuranga, Chuki Hassan, amefariki dunia baada ya lori la mchanga kumkanyaga akiwa kwenye usafiri wa bodaboda waliopanda 'mishkaki', wakati akikimbizwa hospitali ya wilaya ya Mkuranga kujifungua lakini mtoto wake yuko hai baada ya tumbo kupasuka na mtoto kuokotwa pembezoni mwa barabara akiwa hai.
Dk Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha ST Vincent Vikindu, DK Alberto Adolph amethibitisha mtoto huyo kuwa hai ambaye walimpatia huduma ya kwanza ya watoto, mara baada ya kuzaliwa na anaendelea vizuri na tayari amekwishachukuliwa na ndugu zake.
ITV imefika nyumbani kwa marehemu Chuki na kushuhudia mtoto mchanga ambaye kwa sasa atalelewa na mama yake mdogo aitwaye Fatuma Hassan.
Hata hivyo, Fatuma ameiomba jamii na wadau kwa ujumla walioguswa na tukio hilo kumsaidia mtoto mahitaji mbalimbali ikiwemo maziwa kwa kuwa yeye hali yake kimaisha si nzuri na mwenye kuguswa amtafute kutumia namba yake ya simu ya mkononi 0676 846679.
Baadhi ya wakazi waliohudhuria maziko ya Bi Chuki, wameiomba Serikali kuboresha miundombinu rafiki ya barabara, huduma za kijamii ikiwemo zahanati ili kunusuru maisha ya wananchi wakiwemo mama na watoto ambao wanatembea umbali mrefu kutafuta matibabu.