Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lori lagonga basi dogo, laua watu 6

90403 Ajali+pic Lori lagonga basi dogo, laua watu 6

Tue, 31 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Watu sita wamefariki papohapo na wengine 12 kujeruhiwa katika ajali ya basi dogo aina ya Toyota Coaster kugongana na lori aina ya Mitsubishi Fuso katika eneo ambalo wakazi wanasema limekuwa na ajali za mara kwa mara.

Ajali hiyo ilitokea juzi saa 4:00 usiku mita chache kabla ya kufika kituo cha mwisho Nzuguni ambako lilikuwa likienda kutoka eneo la Sabasaba na abiria wamesema walikuwa katika mwendo wa taratibu, lakini lori lililokuwa katika mwendo wa kasi likahamia upande wao barabarani na kusababisha ajali hiyo.

Mganga mfawidhi wa mkoa, Dk Ernest Ibenzi alisema walipokea miili ya watu sita pamoja na majeruhi wengi, lakini akasema waliolazwa walikuwa 12 wakati wengine walichunguzwa na kuruhusiwa.

“Kati ya miili hiyo, watatu ni wanaume na mwili mmoja ni wa mama mtu mzima, wale wagonjwa tunaendelea kuwahudumia na hali zao si mbaya sana. Tuendelee kuwaombea,” alisema Dk Ibenzi.

Kamanda wa polisi wa mkoa, Gilles Muroto hakupatikana na baadaye alituma taarifa kuwa alikuwa mgonjwa.

Mmoja wa watu waliokuwepo kwenye gari lililopata ajali, Zahoro Stephen alisema kilichowasaidia kutoka salama ni ujasiri wa dereva wa Coaster na Mungu, vinginevyo wangekwisha wote.

Stephen, ambaye ni muuza matunda katika soko la Sabasaba, alisema ajali ilitokea wakiwa katika mwendo mdogo kwa kuwa walikuwa wamekaribia kufika kona ya kuingia kituo cha mwisho.

Alisema basi hilo liliondoka kituo cha Sabasaba likiwa limejaza abiria, lakini walishuka kadri lilivyokuwa linakaribia Nzuguni na wakati wa ajali kulikuwa na watu wapatao 20.

Mfanyabiashara huyo ambaye alipoteza kijana wake anayeitwa Omar Mdira (16) alisema alishuhudia lori likiwa na mwendo mkali na lilihama upande wake kwenda walikokuwa na kuwagonga, likifumua eneo la juu la bodi ya gari yao.

Lakini historia ya ajali za mara kwa mara katika eneo hilo si nzuri.

Ajali ya mwisho eneo hilo ilitokea Oktoba 24 wakati mwendesha pikipiki, Charles Kanyopaa (45) mkazi wa Nzuguni alipopoteza maisha baada ya kugongwa na gari.

Mita chache kutoka eneo hilo, mwishoni mwa 2016 ilitokea ajali iliyohusisha gari dogo lililokuwa likiendeshwa na askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania. Watu watatu walipoteza maisha. Na mwaka 2017 mwanafunzi wa shule alifariki dunia kwa kugongwa na gari akiwa kwenye pikipiki alipokuwa anakimbilia gari la shule.

Mwaka 1996, ng’ombe 29 mali ya mmoja wa marehemu waliofariki dunia katika ajali ya jana, waligongwa na gari na kufa katika eneo hilo ambalo liko mita chache kutoka mahali inapojengwa stendi kuu ya mabasi ya mkoa.

Ng’ombe hao walikuwa mali ya Chilangazi Machite (47) ambaye juzi alipoteza maisha akitokea mjini huku mke wake akipata majeraha na hadi jana alikuwa wodi namba 16 katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Diwani wa kata hiyo, Aloyce Luhega alisema katika eneo hilo kunapaswa kuangaliwa kwa kuwa kumekuwa na ajali za mara kwa mara ambazo zinagharimu maisha ya watu na mali zao.

Luhega alisema ajali hiyo ni somo, hasa kwa viongozi kwa kuwa kuna miili imechukua muda kutambulika kutokana na wapangaji wa eneo lake kutokuwa na utambulisho kamili na hadi jana mwili mmoja wa mwanaume haukuwa umetambuliwa.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nzuguni C, Idrisa Bale alisema jana ajali hiyo ilihusisha watu watatu kutoka mtaa wake.

“Katika mtaa wangu watu wawili wamefariki lakini kuna yule kijana (Omar Mdila -16) yeye ni mgeni pale na mwili wake umepelekwa Kondoa hivyo tumeguswa sana na tukio hili,” alisema Bale ambaye Coaster ingeishia mtaani kwake.

Chanzo: mwananchi.co.tz