Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Liwale waambiwa baada ya Corona ni kupimwa mimba

Tue, 28 Apr 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SASA ni wazi kwamba mabinti wa shule zote 17 za sekondari wilayani Liwale mkoani Lindi, watapimwa mimba watakapomaliza likizo ya kuzuia kusambaa virusi vya corona.

Kabla ya kufanyika uamuzi huo, wanafunzi 13 walikutwa na mimba katika upimaji uliofanyika kuanzia Januari, mwaka huu mara tu waliporudi shuleni baada ya kumaliza likizo ya Desemba mwaka jana.

Katika mazungumzo yake na gazeti hilo, Mkuu wa wilaya hiyo, Sarah Chiwamba, anasema wanafunzi walitokana na mimba hizo nyumbani kwao walipokuwa likizo ya Desemba na kwamba baadhi ya shule ambazo wanafunzi walipimwa na kukutwa na ujauzito kuwa ni Rashid Mfaume Kawawa, Lawale Day, Barikiwa, Mihumo na Kiangara.

"Sasa wapo likizo ambayo bado hatujajua itaisha lini, na kwa sababu mimba walizokutwa nazo walitoka nazo kwao, watakaporudi shule itabidi kazi ya kuwapima wote ianze upya," anasema Chiwamba.

Anasema, ni jukumu la wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanakuwa salama wakati wote wa likizo, kwa sababu wako mikononi mwao, na kwamba wakizembea, watasababisha kuendelea kuwapo mimba.

"Lakini pia sisi tutalazimika kuwapima upya, kwa sababu wale waliokutwa na mimba walipata wakiwa likizo, hivyo huenda likizo hii nayo wakapatikana wengine wenye mimba," anasema.

Anasema, wao kama serikali wanalazimika kufanya hivyo ili kujiridhisha kama wanafunzi walikuwa salama huko nyumbani kwao, na kusisitiza kuwa kila mzazi na mlezi awe makini na mtoto wake.

VYANZO VYA MIMBA

Mmoja wa wakazi wa Liwale, Bakari Chikojo anasema, kuna sababu mbalimbali zinazochangia kuwapo kwa mimba na hata ndoa za utotoni, mojawapo ikiwa kiwango kidogo cha elimu ya afya ya uzazi na wazazi.

Anasema baadhi ya wazazi hawazungumzi na watoto wao kuhusu masuala ya uzazi na kwamba mtoto anapoanza kupata mabadiliko ya mwili, hivyo wazazi wanatakiwa kuzungumza naye.

"Vilevile kuna suala la umasIkini, tamaa, kufanya ngono zembe, shinikizo rika na mambo ya mila na desturi, vyote hivyo na mengine mengi ni miongoni mwa sababu za kuwapo mimba hizo," anasema Chikojo.

Anasema, amewahi kufanya kazi katika asasi moja ya kiraia inayojishughulisha na mambo ya malezi, hivyo anataja sababu ambazo ana uhakika nazo kuwa zinachangia baadhi ya wanafunzi kupata mimba.

"Mambo ya unyago hayana ubaya, lakini nayo yanachangia kuwapo kwa mimba, kwani watoto wa kike wanayofundishwa unyagoji, baadhi yao huyafanyia majaribio na kujikuta wanapata mimba," anasema.

Naye mkazi mwingine wa Liwale, aliyejitambulisha kwa jina la Fatma Machongwe, anasema, wazazi na walezi wakisimamia nafasi zao vizuri, wanaweza kuwa na mchango mkubwa wa kupunguza mimba hizo.

"Wapo baadhi ya wazazi wanachukulia mimba za wanafunzi au ndoa za utotoni kama jambo la kawaida na kumbe ni tatizo, ambalo wanatakiwa kusaidia kulipiga vita," anasema Fatma.

Fatma anasema, taifa linapoteza nguvukazi yake ya baadaye kutokana na wanafunzi kupata ujauzito na kuacha shule, hali ambayo ni sawa na kukatisha malengo yao waliojiwekea.

Anamtaka kila mzazi au mlezi kusimama kwenye nafasi yake kuhakikisha mtoto wa kike hakutani na kikwazo chochote ambacho kinaweza kukatisha malengo yake ya baadaye kwenye elimu.

MIKAKATI KUDHIBITI

Mkuu wa Wilaya, Sarah Chiwamba anasema, katika jitihada za kukabiliana na tatizo la mimba na ndoa za utotoni, wana mkakati wa kuanzisha klabu za wanafunzi kila shule zitakazosaidia kutoa elimu ya uzazi na mambo mengine muhimu.

Anasema, klabu hizo za kuwakutanisha wanafunzi wa kike na wa kiume ni za muhimu kwa vile zinaweza kuwa na mchango mkubwa wa kuwaweka vijana hao sawa pale wanapokutana kubadilishana mawazo.

Mkuu huyo wa wilaya anasema, kwa kukutana kwao na kujadiliana mambo mbalimbali yanayohusu masomo na hata makuzi, kunaweza kuwatoa kwenye mawazo ya kufikiria mambo ya uhusiano wa kimapenzi.

"Ninasema hivyo kwani hatua hii inaambatana na kutoa elimu ya uzazi na masuala mengine ili kumsaidia mtoto wa kike kujiamini kama njia mojawapo ya kumaliza matatizo yakiwamo ya ukatili wa kijinsia," anasema.

Anasema, kwa kutambua tatizo hilo, serikali wilayani Liwale pia inashirikiana na mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali kuendelea kufanya jitahidi za dhati za kuhakikisha inatokomeza tatizo hilo.

"Tumeanzisha pia mikakati mbalimbali ya utoaji elimu kwa jamii ya Liwale hasa wazazi juu ya madhara ya ndoa za utotoni kwa mtoto wa kike na umuhimu na haki ya mtoto wa kike ya kusoma," anasema.

Anasema, jamii inatakiwa imthamini mtoto wa kike na kulinda afya yake kwa kumuepusha na mimba na hata ndoa za utotoni ili aweze kusoma bila kikwazo chochote njiani.

MADHARA

Anasema, yeye siyo mtaalamu wa afya, lakini anafafanua kuwa kuna ushahidi wa kutosha wa kisayansi kwamba mimba na ndoa katika umri mdogo kwa msichana chini ya umri wa miaka 18, ni hatari kiafya.

"Chini ya umri huo, mtoto bado hajawa tayari kuyakabili majukumu ya uzazi na unyumba, hivyo ni mateso tu kwake, ndiyo maana mimba hizi na ndoa vinapigwa vita kila kona nchini," anasema.

Anasema, kwa hali yoyote, kuna haja ya kukomesha tatizo hilo la mimba na ndoa za utotoni ili kuwalinda watoto wa kike, kwa vile mimba pia ni kinyume na haki za binadamu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live