Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lindi na Mtwara yaingiza Sh 162.9 bilioni za mauzo ya ufuta

69775 Lindi+pic%255C

Sun, 4 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Lindi. Mikoa ya Lindi na Mtwara imeingiza Sh162.9 bilioni zitokanazo na mauzo ya zao la ufuta kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.

Kilo moja ya ufuta imeuzwa kati ya Sh2,650 hadi Sh3,100 kwa msimu wa mwaka 2018/2019 .

Hadi kufikia jana Jumamosi, Agosti 3, 2019, mikoa hiyo imeshauza ufuta tani 59,208, Mkoa wa Lindi ukiwa kinara kwa kuuza tani 52,232 na kuingiza Sh144.6 bilioni na Mtwara ukiuza tani 6,975 na kuingiza Sh18.2 bilioni.

Akisoma taarifa ya mikoa ya kusini katika ufunguzi wa maonyesho ya Nanenane kanda ya kusini, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga amesema kutokana na mauzo hayo, halmashauri 15 za mikoa hiyo zimeingiza zaidi ya Sh4.9 bilioni.

“Lindi tumeingiza Sh4.3 bilioni na Mtwara Sh377.7 milioni , niwapongeze wakulima kwa kuendelea kuiamini Serikali na kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani, ambao kwa kiasi kikubwa umesaidia kusimamia kazi ya  ukusanyaji wa ufuta mpaka kuuzwa,” amesema Shaibu.

Mkuu wa wilaya ya Masasi, Selemani Mzee akifungua maonyesho hayo kwa niaba ya mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), amesema Bajeti ya 2019/20 iliyopitishwa na Bunge, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imetengewa Sh318.4 bilioni.

Pia Soma

“Kilimo pekee kimetengewa Sh253.8 bilioni, Mifugo na Uvivu Sh64.9 bilioni ikilinganishwa na mwaka wa fedha wa 2018/19 zilitengewa 26.7 bilioni. Kwa hiyo hapa kuna ongezeko kubwa la bajeti,” amesema Mzee.

Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Naliendele, Dk Fortunatus Kapinga amesema zao la ufuta linaweza kulimwa zaidi ya mara moja kwa mwaka kama kutakuwa na uwezekano wa kumwagilia.

“Katika kituo chetu tuna shamba la kuzalisha mbegu lakini tunazalisha kwa njia ya umwagiliaji na unaweza kuvuna mbegu kwa mwaka mzima, sasa kwa wakulima kinachohitajika ni kuwa na uwezekano wa kuwa na umwagiliaji,” amesema Dk Kapinga.

Chanzo: mwananchi.co.tz