Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Linda na kudumisha uwezo wako wa kusikia

66e08d15ecbb4873da24540202c0ac21 Linda na kudumisha uwezo wako wa kusikia

Tue, 22 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

UWEZO wa kusikia ni zawadi kutoka kwa Mungu inayopaswa kuthaminiwa, lakini kadiri mtu anavyozeeka ndipo uwezo wake wa kusikia unavyopungua.

Ulimwengu wa sasa huambatana na sauti nyingi tofauti na kelele ambazo zinachangia kuharibu uwezo wa mwanadamu kusikia hata kabla ya uzee.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) zaidi ya watu milioni 120 ulimwenguni wana matatizo ya kusikia wakiwemo vijana.

Mwanasayansi kutoka Taasisi Kuu ya Viziwi huko St. Louis, Missouri, Marekani, Margaret Cheesman, anasema: “Karibu robo tatu ya matatizo ya kusikia ambayo Mmarekani mmoja yanamkabili yanatokana na yale ambayo amesikiliza maishani mwake na siyo kwa sababu ya uzee.”

Anasema mara nyingi matatizo ya kusikia husababishwa na kazi zenye kelele unazosikia wakati unapofanya mambo unayoyapenda ikiwemo miziki.

Daktari Cheesman anasema kusikiliza sauti kubwa, hata kama ni kwa muda mfupi kwaweza kuharibu sehemu nyororo za ndani za sikio lako.

Kila siku watu wengi wanakabiliana na sauti za aina tofauti kuanzia za magari hadi sauti za juu za mashine za umeme kazini.

Licha ya hayo, anasema wakati mwingine mwaadamu mwenyewe huzidisha tatizo hili kwa kuweka sauti za juu katika vifaa anavyosikiliza.

Njia moja wapo anasema ni kusikiliza muziki inayopendwa na wengi hususani vijana kwa kutumia spika za masikioni (earphones).

Marshall Chasin, mmoja wa waanzilishi wa vyama vya wanamuziki vya Canada anasema akikariri uchunguzi uliofanywa nchini Marekani kwamba vijana wengi siku wanaendelea kupoteza uwezo wao wa kusikia kutokana na kutumia spika za masikioni au zinazovaliwa kichwani (headphone) huku wakiweka sauti ya juu kupita kiasi.

Bado wataalamu wa sauti wanasema, kadiri unavyosikiliza sauti inayozidi desibeli 85, ndivyo unavyokabiliwa na uwezekano mkubwa wa kupoteza uwezo wako wa kusikia.

Ingawa mtu anaweza kuzaliwa na matatizo ya kusikia ama akayapata kupitia maradhi yasiyotazamiwa, tunaweza kujitahidi kulinda na kudumisha uwezo wetu wa kusikia kwa kujitenga na kusikiliza sauti za juu.

Mtaalamu mmoja wa sauti anasema: “Kungojea mpaka tatizo litokee ndipo uchukue hatua ni kama kuanza kutumia kifaa cha kuzuia mbu baada ya kuambukizwa malaria.”

Anasema iwapo redio katika gari lako au nyumbani mwako imefunguliwa sauti ya juu na huwezi kusikia mtu anapozungumza, hiyo ni ishara kwamba sauti hiyo imepita kiasi na inaweza kuharibu uwezo wako wa kusikia.

Wataalamu wa usikivu wa sauti wameonya kusikiliza sauti inayofikia desibeli 90 kwa muda wa saa mbili au tatu mfululizo kwamba kunaweza kuharibu masikio yako. Katika baadhi ya mazingira wanapendekeza kuvaliwa kwa vifaa vya kulinda masikio.

Teknolojia ya spika za masikioni imepata umaarufu mkubwa kwa vijana huku wengi wao wakitumia kusikiliza muziki na redio mahali popote walipo kwa kutumia simu au redio.

Watafiti hao wanasema spika za masikioni haziathiri tu ubongo na umakini barabarani, bali inaweza kuwa chanzo cha matatizo ya kusikia ikiwa zitatumiwa kupita kawaida.

Kwa kutumia spika za masikioni, mfumo wa usikilizaji unaanzia sikio la kati, na hivyo zinachosha ngoma ya sikio yenye uwezo wake wa kung’amua masafa ya sauti na pale zinapozidiwa, ndipo kuchoka kwake kunaanza.

Watafiti kuhusu Athari za Kelele kwa Usikivu wa Binadamu Mahala pa kazi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) wanasema matumizi ya muda mrefu ya spika za masikioni na za kichwani (headphone) ni hatari kwa afya ya masikio.

Mtafiti wa Mradi wa Norhed wa Athari za Kelele kwa Usikivu wa Binadamu Mahala pa kazi wa chuo kikuu hicho, Dk Israel Nyarubela, anasema utafiti wa wa hivi karibuni umeonesha kuwa hilo ni janga linalowapata vijana kwa wingi na kusababisha uwezo wao wa kusikia kupungua taratibu.

Dk Nyarubela anasema kitu ambacho kinapaswa kifahamike ni kwamba madhara ya kelele kwenye usikivu hayatokei mara moja bali taratibu kutokana na kuathiri sehemu ya ndani ya sikio kwa hiyo usikivu unaendelea kupungua bila mtu mtu kung’amua.

“Utafiti unaonesha earphones na headphones si salama sana kuzitumia kwa muda mrefu,” anasema Dk Nyarubela.

Anasema tafiti nyingi zimefanyika na kuonesha vifaa hivyo vina madhara kwa watumiaji lakini kwa bahati mbaya imekuja fasheni ya teknolojia hiyo kutumika.

“Tunashauri lazima mtu aelewe sio mbaya ila usishawishiwe na huo muziki, kwani ni kishawishi kwa maana unashawishika kuongeza sauti bila kujua kuwa kesho na kesho kutwa yako usikivu wako utapungua,” anasema Dk Nyarubela.

Kadhalika anasema kuthibiti kiwango salama cha sauti ambacho hakiwezi kuleta madhara kwa masikio ni changamoto kubwa sana.

“Najua ya kwamba kuna kiwango ambacho kimewekwa hapa nchini na Shirika la Viwango Tanzania ambacho ni sauti isiyozidi desibeli 85 lakini kiwango hicho bado kinaweza kuleta madhara,” anasema Dk Nyarubela.

Dk Nyarubela anasema ukiingia kwenye baadhi ya baa utasikia kelele kubwa sana inayoleta karaha lakini baada ya muda utahisi sauti inakuwa ya kawaida kutokana na mwili kufanya kazi ya kuizoea hali hiyo.

“Lakini ukumbuke hakuna kilichobadilika sauti ni kubwa vile vile na unapoendelea kuishi kwenye mazingira hayo usikivu wako unanza kuathirika taratibu,” anasema Dk Nyarubela.

Dk Nyarubela anasema kwenye matamasha yanayofanyika wanamuziki wengi wa nje ya nchi wamefanyiwa tafiti hizi na wengi wakagudulika kuwa na shida za usikivu,” anasema.

Katika nchi zilizoendelea kwa sasa wanamuziki wengi wanavaa spika za kivchwani zenye kifaa maalumu cha kurekebisha sauti na sio sauti iliyopo ukumbini.

Anasema hiyo ilikuja baada ya kubainika wanamuziki wengi wa zamani waliathirika usikuvu wao kwa sababu ya mlio mkubwa wa sauti.

“Kwa sasa wamekuja na taaluma mpya na unaweza kuwaona wanamuziki wamevaa hizo headphone na watu wengine wakadhani ni fasheni, sio bali wataalamu wamepima sikio lake,” anasema Dk Nyarubela.

Anaongeza: “Wataalamu wakishampima mwanamuziki wanakwenda kiwandani kumtengenezea kifaa hicho kulingana na kipimo chake halisi na kukitumia kwenye matamasha yake anapopanda jukwaani na ili kulinda usikivu.”

Kutokana na madhara yanayojitokeza kupitia tafiti zilizofanyika, Muhas imepata vifaa vya kisasa vya kufundishia na kufanyia utafiti na kimepata kifaa cha kisasa cha kupima kiwango cha usikivu kwa wafanyakazi mahapa pa kazi.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Profesa Andrew Pembe anasema Tanzania sasa inaenda kwenye uchumi wa viwanda na kasi ni kubwa hivyo ni wajibu sehemu za kazi na sehemu za viwanda kuwa salama dhidi ya sauti kali kwa wafanyakazi.

“Tikiweka usalama zaidi kwenye eneo hili tutakuwa tumechangia kwenye lengo kuu la Taifa letu kwenda kwenye uchumi wa viwanda na wananchi wa Tanzania wakiwa na afya njema,” anasema Profesa Pembe.

Anasema kazi ya vyuo vikuu ni kuzalisha rasilimali watu na kufanya tafiti za kisanyansi ambazo zitawezesha kuboresha fani mbalimbali pamoja na kutoa ushauri elekezi katika kuzishauri Serikali na taasisi mbalimbali.

Profesa Pembe, anasema ushirikiano wao na vingine viwili; cha Addis Ababa, Ethiopia na Chuo Kikuu Bergen cha Norway, umeinufaisha Muhas kwa kupatiwa kifaa cha kisasa cha kupima sauti katika masikio ili kubaini wale wanaopata matatizo ya sikio kutokana na kelele za kwenye viwanda wakati wa uzalishaji.

Makamu mkuu huyo wa chuo anasema ushirikiano uliopo kwa miaka mitano umekiwezesha chuo hicho kuhakikisha kinafanya vizuri kuwajenga kitaaluma wataalamu wake.

“Kwa kipindi cha miaka mitano kuna mengi ambayo yamefanyika lakini cha muhimu zaidi katika kushirikiana huku ambako kumetokea tumeboresha mitaala yetu ambayo inahusu usalama sehemu za kazi,” anasema.

Anasema kutokana na ushirikiano huo Muhas imepata fursa ya kusomesha watu 39 kwenye shahada ya uzamili na wanne kwenye program ya Post Doctoral.

Naye Mkuu wa Mradi wa Kupunguza Maumivu na magonjwa yatokanayo na mahala pa kazi wa Chuo Kikuu hicho, Profesa Simon Mamuya, anasema baada ya nchi yetu kujielekeza kwenye uchumi wa viwanda, chuo kikuu hicho kiliona ni muhimu kuweka mazingira ya uotaji wa elimu katika eneo hilo.

Anasema hatua nyingine ni kufanya utafiti kwenye viwanda na migodini kwa lengo ya kuwafanya wananchi washiriki vyema kwenye ujenzi wa uchumi wa taifa wakiwa wenye afya njema na salama.

“Eneo la afya na usalama mahala pa kazi bado halijapewa kipaumbele zaidi, tumeacha ile afya na tumejikita zaidi eneo la usalama kazini,” anasema Profesa Mamuya.

Mkuu huyo wa Mradi wa Kupunguza Maumivu na Magonjwa yatokanayo na mahala pa kazi wa chuo kikuu hicho anasema: “hatujaagalia magonjwa yanayoweza kuwapata wafanyakazi, hivyo ni vyema wanyakazi wakafanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara wa afya zao ili kubaini viasharia vya magonjwa na kuwakinga.”

Chanzo: habarileo.co.tz