Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Likizo ya corona yasababisha mimba 42

6b19eb05b3742a30e97121176670de4e Likizo ya corona yasababisha mimba 42

Thu, 10 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WILAYA ya Kasulu mkoani Kigoma imetajwa kuongoza kwa matukio mengi ya ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto ambapo katika kipindi cha janga la corona pekee watoto 42 walipata ujauzito na kukatiza masomo yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kivulini, Yassin Ally, aliyasema hayo wakati wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Umoja mjini Kasulu.

Alisema wilaya hiyo ina idadi kubwa ya kesi za kijamii ambapo wanaume huwapiga wake zao na ndoa kuvunjika.

Ally alisema kuwa pamoja na wanaume kupiga wake zao na ndoa kuvunjika, wazazi pia hawasimamii kwa karibu malezi, matunzo na ulinzi kwa watoto waojambo ambalo limekuwa na athari kubwa kwa jamii na kusababisha watoto wengi kupata ujauzito.

Naye Mtendaji Kata ya Marubona, Hussein Kapwacha, alisema baadhi ya wazazi wa wilaya hiyo wanakasumba ya kwenda mashambani umbali wa kilometa 40 hadi 60 na kuacha watoto peke yao kwa zaidi ya miezi sita hali inayosababisha watoto kujilea wenyewe na kuwafanya wapate ujauzito katika umri mdogo.

Mkuu wa Dawati la Jinsia la Polisi Wilaya ya Kasulu, Maimuna Abdul, alisema changamoto wanazokutana nazo ni pamoja na kutekeleza majukumu yoa kwa ufanisi kutokana na waathirika kutofika kituo cha polisi kwa wakati, ushirikiano mdogo kutoka kwa waathirika na wakati mwingine kuharibu ushahidi, kushindwa kufika mahakamani na hofu ya kuvunja uhusiano kutokana na waathirika na watuhumiwa kutoka familia moja.

Alisema jumla ya kesi 153 za watoto zimepokelewa mwaka huu, kesi za watoto zilizopo mahakamani zipo 20, kesi zilizopo chini ya upelelezi 133, kesi za mimba 42 baada ya corona, ndoa za utotoni 7, kesi za ukatili wa kijinsia za watu wazima 333 na kati ya hizo 43 zipo mahakamani na 290 zipo chini ya upelelezi.

Makamu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya wanwake (UN Women), Julia Broussard, alisema kuwa ukatili wa kijinsia hapa nchini umeathiri idadi kubwa ya wanawake na wasichana kutokana na utafiti wa afya ambapo katika mwaka 2016 asilimia 40 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 19 wamenyanyasika na asilimia 17 walipata unyanyasaji kwa miezi 12 iliyopita.

Chanzo: habarileo.co.tz