Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lami baridi yafanyiwa majaribio Dodoma

5900878d91db55a2a25abd906689e763 Lami baridi yafanyiwa majaribio Dodoma

Thu, 23 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

UJENZI wa barabara darasa kwa kutumia teknolojia ya lami baridi umeanza jijini hapa huku Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) ikisema iwapo teknolojia hiyo itaonekana kufanya vizuri watairuhusu iweze kutumika maeneo mbalimbali nchini.

Kampuni ya Starpeco Limited ya Jijini Dar es Salaam ndio watekelezaji wa mradi huo. Hayo yalielezwa juzi na Meneja wa Tarura Mkoa wa Dodoma, Mohammed Makwata wakati akifungua semina ya wanafunzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi (Veta) nchini ambao walikuwa wakipewa uelewa kuhusu teknolojia ya lami baridi.

Semina hiyo iliandaliwa na Kampuni ya Starpeco Limited ya Jijini Dar es Salaam ambayo inajishughulisha na ujenzi wa barabara kwa kutumia lami baridi. Meneja huyo wa Tarura Dodoma, alisema iwapo teknolojia ya lami baridi itaonekana kufanya vizuri watairuhusu iweze kutumika maeneo mbalimbali nchini kwani wana mtandao mkubwa wa barabara.

“Teknolojia hii ikionekana kufanya vyema basi itatumika katika ujenzi wa barabara zetu. Tarura ina barabara nyingi zinazohitaji kujengwa na kutumika nyakati zote kwa maendeleo ya uchumi wa nchi,”alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni Starpeco Limited, Gratian Nshekanabo alisema kampuni yake imeweza kuweka viraka katika barabara ya Changanyikeni na barabara ya Uvumbuzi zilizopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), pamoja na kumwaga lami mpya katika barabara ya Kileleni yenye urefu wa kilomita 120.

Alisema teknolojia ya lami baridi imetumika katika ujenzi wa barabara ya Bagamoyo, Daraja la Juu la Tazara na Ubungo ambapo kwa sasa wanakarabati barabara darasa katika Jiji la Dodoma.

Alizitaja barabara hizo ni zile zenye majina ya viongozi wakuu wa nchi ambazo ni ya Magufuli na Samia zilizopo Area C. Mkurugenzi huyo alisema teknolojia hiyo ni nzuri kwa kuwa ni rafiki kwa mazingira, ni rahisi na gharama zake ni ndogo hivyo aliitaka serikali kuitumia katika ujenzi wa barabara zake.

“Kwenye ujenzi wa lami kuna faida nyingi na ni rafiki kwa mazingira, ni rahisi tuache mazoea kwani mambo yamebadilika tunaweza tukawa tunawalalamikia wakandarasi wakati hawatakiwi kulalamikiwa, tubadilike tutumie lami baridi,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz