Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

LAAC yashtushwa na deni la Sh45 bilioni Halmashauri Shinyanga

FEDHA APRIL 0 LAAC yashtushwa na deni la Sh45 bilioni Halmashauri Shinyanga

Fri, 22 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC), imesema deni la Sh45 bilioni inayodaiwa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ni kubwa na halmashauri hiyo haiwezi kulilipa.

Hatua hiyo inakuja wakati Oktoba 20, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilisema PSSSF ina madai mengi katika taasisi mbalimbali ambayo ni makato ya watumishi hivyo kuufanya kushindwa kujiendesha vizuri.

Akizungumza jana Alhamisi Oktoba 21 bungeni jijini Dodoma, kuhusu deni la Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Seleman Zedi amesema deni hilo walilibaini baada ya kufanya uchambuzi wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka unaoishia Juni 30 mwaka 2020.

Zedi amefafanua kuwa deni hilo limefikia kiwango hicho kutokana na adhabu ya kuchelewa kupeleka makato ya michango ya wafanyakazi kwenye mfuko huo.

Hofu ya kamati kuhusiana na deni hilo inatokana na ufinyu wa mapato ya halmashauri hiyo ambayo ni Sh2 bilioni kwa mwaka huku deni likiwa ni Sh45 bilioni.

Ameagiza wakae PSSSF na Hazina waangalie jinsi watakavyotazama adhabu wanayopewa kutokana na kushindwa kuwasilisha makato hayo ya watumishi wa umma kwa wakati katika mfuko huo.

Amewataka kuongeza kiwango cha malipo ya deni hilo ili kuwafanya PSSSF katika mazungumzo yao wahamasike kuwaondolea adhabu hiyo.

“Ongezeni malipo hayo kwa sababu sasa kiwango cha mapato yenu kinaimarika zaidi. Hili ni fundisho kwa sababu chanzo ni halmashauri kutopeleka michango kwenye mifuko ya hifadhi,” amesema.

Amewataka kuanzia hivi sasa wanapokata michango ya watumishi kutoka kwenye mishahara yao, wahakikishe inapelekwa kwa wakati kwenye mfuko huo ili kuepuka adhabu kwa sababu sheria iliyopo ina adhabu nyingi.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Zuwena Omary ambaye alikuwapo kwenye kikao hicho na kamati, ameiahidi kamati kwamba wataenda kushirikiana na viongozi wengine kuhakikisha kuwa hawarudi walikotoka.

Naye Mwenyekiti wa LAAC, Grace Tendega akitoa maoni ya jumla baada ya kufanya uchambuzi kwenye halmashauri hizo alisema changamoto kubwa inayoonekana ni kutotenga fedha za maendeleo kama inavyotakiwa katika miongozo ya Tamisemi.

Nyingine ni kutotengwa kwa fedha za mfuko wa wanawake, vijana na wenye ulemavu na kutorudishwa vijijini kwa asilimia 20 ya fedha zinazotolewa na Hazina.

Chanzo: mwananchidigital