Ukara. Wakati Serikali imetangaza kukamilika kwa operesheni ya uokoaji na uopoaji miili katika ajali ya Mv Nyerere, baadhi ya watu wamejitokeza wakidai kutopata miili ya ndugu zao licha uhakika kuwa walikuwamo ndani ya kivuko.
Wakizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana, watu hao walisema tangazo la kukamilika kwa operesheni ya uokoaji limewaacha bila uhakika wa kupatikana kwa miili ya ndugu zao.
“Serikali inatakiwa kuliangalia suala hili la kutangaza mwisho wa operesheni kwa makini kwa sababu linazidisha huzuni na simanzi kwetu ambao licha ya uhakika kuwa ndugu zetu walikuwamo kwenye meli (kivuko), miili yao haijapatikana,” alisema mzee Buhatwa Masyenene.
Mzee Masyenene, mkazi wa kijiji cha Nyamanga Kisiwa cha Ukara alisema hadi operesheni hiyo ilipohitimishwa Septemba 28, hakuwa amapata mwili wa mke wake, Veronica Buhatwa (43) aliyekuwa ndani ya kivuko.
“Pamoja na mke wangu, ndugu wengine waliokiwamo ndani ya kivuko ambao wote wamenusurika ni Ndalo Maligila, Sanday Marwa, Restuta Mgeta na Neema Zakayo,” alisema Masyenene na kuongeza:
“Ndalo ndiye aliyemkatia mke wangu tiketi ya kivuko na wakapanda wote.”
Mkazi mwingine aliyejitokeza akidai kutopatikana kwa mwili wa ndugu yake ni Chamkaga Rwegano wa kijiji cha Igongo kilichopo kisiwa cha Ukerewe aliyempoteza mdogo wake, Paschal Rwegano (30).
Rwegano alisema siku ya tukio, mdogo wake ambaye ni mtaalamu wa kuchana mbao alikuwa na mwenzake aliyemtaja kwa jina la Sosthenes Bangili, mkazi wa Igongo ambaye mwili wake ni kati ya 230 ya waliokufa kwenye ajali hiyo iliyoopolewa majini.
“Kutopatikana kwa mwili wa mdogo wangu kumetuweka njia panda kama familia tusijue la kufanya; ni heri angepatikana tumzike kwa heshima tujue amekufa kuliko hali hii,” alisema.
Pia, kilio kama hicho kimetolewa na Mkanya Mbogo aliyesema hadi tangazo la kisitisha operesheni ya uokoaji linatolewa, mwili wa dada yake, Veronica Mbogo (38) haukuwa umepatikana.
Akizungumzia uhakika wa Veronica kuwa miongoni mwa waliokufa, Prisca Mwesa, binamu yake waliyekuwa wote ndani ya kivuko alisema muda mfupi kabla ya ajali walikuwa wameketi pamoja.
“Tangu ajali ilipotokea Alhamisi hajaonekana wala simu yake ya mkononi haipatikani,” alisema.
Baba mdogo wa Veronica, Juma Msusa alisema familia inakusudia kuweka matanga wanaamini amekufa kwenye ajali hiyo.
Kauli ya Serikali
Mwenyekiti w Kamati ya Maafa ya Mv Nyerere, Isack Kamwelwe ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi alisema juzi kuwa baada ya kivuko hicho kunyanyuliwa na kvutwa hadi ifukwe wa Ziwa Victoria katika kijiji cha Bwisya kisiwa cha Ukara, hakuna mwili uliokutwa ndani.
Kuhusu madai ya baadhi ya watu kutopata miili ya ndugu zao, Kamwelwe alisema inawezekana miili hiyo imesambazwa na kusukumiwa mbali na upepo na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi katika hatua zote zilizosalia.