Mwanza. Kutokana na kujirudia kwa matukio ya makundi ya ndege kuvamia ndege za abiria zikiwa zinatua Uwanja wa Ndege wa Mwanza, uongozi wa uwanja huo umeeleza mkakati wa kukabiliana na hali hiyo.
Akizungumza na Mwananchi jana Alhamisi Desemba 13, 2018 meneja wa uwanja huo, Maulid Mohamed amesema ndege hao ambao muda mwingi wanazunguka uwanjani hapo kwa sasa wanawafukuza kwa kutumia magari maalumu.
Amesema watu wamewekwa kwa ajili ya kuwafukuza ndege hao ili kuhakikisha hawapo eneo la uwanja wakati ndege ikitua na kwamba, wahusika hupewa ishara kutoka kwa muongoza ndege.
Makundi ya ndege hao kwa nyakati tofauti yamevamia ndege mbili zilizokuwa zikitua katika uwanja huo na kuzua taharuki.
“Tumeandaa huu mkakati wa kuwatumia watu na magari ili waweze kuwahangaisha ndege hasa wakati ndege zikitua lengo ni kuhakikisha zinatua kwa usalama,” amesema.
Amefafanua kuwa si mara ya kwanza kutokea kwa kundi la ndege hao kwa maelezo kuwa huwa wengi kipindi cha mvua, akieleza kuwa sababu nyingine ni za kijiografia.
“Sasa hivi hata ukienda Uwanja wa Ndege wa Entebbe au Kisumu hali ni kama hii tu ya Mwanza. Tunaamini ndege hai hao watapungua kadri mvua inavyozidi kupungua,” amesema Mohamed.
Maurice Kimune, mmoja wa abiria wa ndege amesema makundi hayo ya ndege ni hatari kwa usalama wa abiria yanapovamia ndege zikitua.
“Ndege hao ni wengi kupita maelezo na wanakuwa wanakimbia hovyo. Rubani anaweza kuchanganyikiwa na kupoteza mwelekeo,” amesema.