Hamasa ya wananchi wanaojiandikisha kuhama kwa hiyari kutoka eneo la hifadhi ya Ngorongoro imeongezeka ambapo leo tarehe 19 February , 2024 jumla ya kaya 82 zenye wananchi 541 na mifugo 3,379 zimehama kutoka Ngorongoro kweda Kijiji cha Msomera Handeni Tanga.
Akizungumza wakati wa kuaga kundi hilo Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Richard Kiiza amesema kuwa baada ya kuhama kwa kundi hilo leo inafanya idadi ya wananchi waliokwishahama ndani ya hifadhi tangu zoezi lilipoanza hadi leo kufikia kaya 1,032 zenye watu 6,395 na mifugo 28,982.
Kamishna Kiiza amebainisha kuwa kadri siku zinavyoenda wananchi wengi wanahamasika na kujiandikisha kuhama kwa hiari yao wenyewe hasa baada ya ushuhuda wa maisha mazuri kwa wananchi wenzao waliokwishatangulia ambao Maisha yao yamebadilika kwa kiasi kikubwa.
“Wananchi waliotangulia mwaka jana wengi wao wamejenga nyumba za kisasa, wamelima mazao ya kutosha kwa ajili ya chakula na biashara, wanamiliki vyombo vya usafiri, wanapata huduma bora za maji, umeme, shule, mawasiliano, huduma za afya, posta, malisho na majosho, hali hii imefanya wao kuwa mabalozi kwa wenzao waliobaki Ngorongoro” ameongeza Kiiza.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Kanali Wilson Sakulo akiwaaga wananchi hao ameeeleza kuwa wananchi wote wanaohama haki zao za msingi zimezingatiwa kwa mujibu wa sheria, na kila kaya inayoondoka inaingiziwa fedha kiasi cha shilingi milioni 10 na fedha zingine za fidia ya maendelezo waliyoyafanya wakiwa Ngorongoro.
Amewahakikishia wananchi hao kubwa mbali na faida na huduma wanazozikuta msomera wakiwa safarini pia Serikali inawapatia ulinzi na escort , huduma ya afya, chakula cha njiani, kusafirishiwa mizigo yao na mifugo yao na wakifika Msomera watakabidhiwa nyumba ya vyumba vitatu iliyoko kwenye eneo la ekari 2.5, shamba la ekari 5 na kupewa mahindi ya chakula kwa kipindi cha miezi 18.