Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kukosa ajira kumemfanya ageukie ufundi seremala

Mon, 24 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni ndoto ya kila muhitimu kupata ajira baada masomo. Kwa bahati mbaya ni asilimia ndogo ya maelfu wanaofanikiwa kuingia katika ajira kila mwaka duniani kote.

Winy Mokami binti mwenye umri wa miaka 28 ni mfano katika kundi la vijana wengi wanaoingia mtaani na kujikuta walichotarajia sicho. Alihitimu Chuo Kikuu cha mtakatifu Agustino (Sauti) jijini Mwanza, mwaka 2015 lakini kama wengine hakutimiza ndoto yake kufanya kazi aliyoichagua kuisomea.

“Nilisoma nikiwa na matumaini ya hali ya juu kwamba nitapata kazi lakini bado sikukaa nyumbani hata baada ya kuhitimu. Siku hizi inafahamika vyema kwamba baada ya kuhitimu, kupata ajira rasmi ni mtihani mgumu sana,” anasema mhitimu huyo wa shahada ya manunuzi.

Kwa kuwa alikuwa na wasiwasi wa idadi kubwa ya wahitimu ambao bado wapo nyumbani bila mwelekeo wakisubiri ajira rasmi, Winy aliamua kutupa ndoano katika ujasiriamali.

“Ilinichukua miezi kadhaa kutafakari kitu ambacho ningekifanya na kuniingizia kipato na mtaji wake pia ungegharimu kiasi gani,” anasema Winy.

Anafunua kwamba alikuwa na changamoto nyingine inayotokana na asili yake kwamba mtoto wa kike ana jukumu la kufanya kazi za nyumbani kama vile, kwenda mtoni, kuosha vyombo na kupika.

Kwa nini useremala?

Anasema kabla ya kifo cha wazazi wake kilichosababishwa na ajali, baba yake, Matiko Mahiri alikuwa fundi seremala ambaye alitengeneza madawati ya shule za msingi, benchi na vitu vidogo vidogo.

Anasema alitambua kwamba kuwa seremala kungevuta wateja wengi ambao wengine, wangekuja kwa ajili ya kuona kazi zake na wengine wangetoa kazi.

Winy, mtoto wa tatu baada ya Thomas, Alex na Gadencia, anasema anamshukuru Mungu kwamba baada ya wazazi wao kufariki, baba yake alikuwa tayari ana wateja wengi ambao walikuwa wameagiza kutengezewa viti vya kanisani, mabenchi kwenye mabanda ya sinema na viti vya nyumbani.

Mafunzo na zana za kufanyia kazi?

Zoezi la kujifunza useremala halikuchukua muda mrefu kwa Winy. Alijifunzia kazi hii kwa mzee mmoja ambaye ni baba mzazi wa rafiki yake, wote walisoma shule moja ya sekondari hapa Tarime.

Matumizi ya randa, msumeno na futi na vitu vingine vidogo vidogo kwenye karakana ya mzee huyo ilikuwa kawaida sana wa Winy.

“Kati ya zana zote pale kwenye karakana, randa ilinichukua siku nyingi ikilinganishwa na vifaa vingine kwa kuwa ni nzito sana na pia kuinyoosha kwenye mbao sio mchezo,” anasema Winy.

Mara kwa mara akiwa pale kwenye karakana ya mzee (mwalimu),alimpa mtihani karibia kila siku ili kumfanyia tathmini ya maendeleo na hatua alizokuwa akipiga.

“Baada ya miezi mitatu, tayari mwalimu alikuwa amekwisha kunikubali kwamba ninaweza na hiyo alikuwa tayari kuniweka huru kama ningekuwa na nia ya kuondoka.”

Wito kwa vijana

Anasema wahitimu wa vyuo wasikae nyumbani wakisubiri ajira rasmi waamke waanze kujishughulisha na hakika Mungu atawafungulia milango.

“Iwapo umekaa nyumbani, kuwa makini sana maana unaweza kuzeeka bila kufanya kitu chochote cha mafanikio. Tuwe wabunifu na hakika tutatoka tu,” anahitimisha.

Chanzo: mwananchi.co.tz