Serikali imesema imekamilisha ratiba na mwongozo mpya wa Serikali na taasisi zake kuhamia Dodoma ambapo mwisho ni mwaka wa fedha 2024/25. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)
Ratiba hiyo imetolewa leo Jumatatu tarehe 16 Januari, 2023 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Suimbachawene, katika hafla ya kukabidhi vibali vya ujenzi taasisi 19 jijini Dodoma.
Simbachawene amesema Waziri Mkuu ambaye ndiye mratibu wa zoezi la kuhamia Dodoma ametoa maelekezo kuwa jumla ya taasisi 42 zitahamia mwaka huu wa fedha 2022/23, taasisi 36 mwaka ujao wa fedha 2023/24 na 19 mwaka 2024/25.
Amesema hadi sasa jumla ya taasisi 65 kati ya taasisi za Serikali 189 za zimeshahamishia shughuli zake Dodoma huku taasisi 55 zikiwa zimejenga ofisi zake na zingine zipo kwenye hatua mbalimbali.
Aidha, ametoa maagizo manne ya kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kama ilivyopangwa ikiwemo kuhakikisha ujenzi wa majengo unakamilika kwa kufuata taratibu zote.
Sera ya kuhamishia makao makuu ya nchi na Serikali Dodoma ilitungwa tangu mwaka 1973 lakini msukumo mkubwa wa utekelezaji wake ulianza katika Serikali ya awamu ya tano chini ya Hayati Dk. John Magufuli na sasa unaendelezwa na Serikali ya awamu ya sita.
Katika utekelezaji huo mwaka 2018 Bunge lilitunga Sheria ya kuitambua Dodoma kuwa makao makuu ya nchi na Serikali.