Wakazi wa kijiji cha Nyabichune kata ya Regicheri na kijiji cha Korotambe kata ya Mwema wametakiwa kuacha chokochoko za ubaguzi wa koo zinazoweza kuhatarisha Amani.
Imeelezwa kuwa wenyeji hao wiki iliyopita walikuwa wamekunjiana ngumi kwa sura ya kutaka kuanza mgogoro wa mapigano ya koo jambo ambalo limelaaniwa vikali na viongozi.
Inadaiwa kuwa baadhi ya wenyeji kutoka kijiji kimoja ambacho hakijabainika waliuza eneo kwa mwekezaji lisilo kuwa la kijiji husika jambo ambalo lilizua mgogoro kwa wenye eneo husika.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mkuu wa wilaya Tarime, Michael Mangwela Mtenjele amekemea vikali sura hiyo na kuwataka wananchi wa Tarime kuacha tabia kama hizo badala yake wafanye shuguli zilizo halali zinazowaingizia kipato.
Mkuu wa wilaya hiyo alitumia nafasi hiyo kuwataka wakazi wa Tarime kupenda wilaya yao na kupenda wenzao hata kama sio wa koo yake pamoja na kufanya shuguli za kimaendeleo zinazoweza kuwaingizia kipato na kuacha kurudisha Tarime kwenye sura ya mapigano ya koo yaliyopitwa na wakati ambayo awali yalisababisha hasara kubwa ya mali ikiwemo mauaji.
"Mimi niseme kuwa mapigano ya koo hayana nafasi kwa sasa naomba wale wote wanaohusika wakiwemo wazee wa mila kuchukua hatua kali dhidi ya wale ambao wanatajwa kuhusika na kama kuna tatizo ipo haja sheria na taratibu kuzingatiwa badala ya kuanza choko choko"alisema Mtenjele.
Kwa upande wake kamanda mkoa wa kipolisi Tarime Rorya,Geoffrey Sarakikya alithibitisha kutokea tukio hilo na kusema wanafuatilia na likiwa tayari waandishi wataambiwa kilichojiri.
Kamanda huyo aliongeza kusema mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Tarime/Rorya (RCO)ameenda kwenye eneo latukio na anashugulikia ili kubaini chanzo ikiwemo wahusika na sheria itachukua mkondo wake.