Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kongamano la uwekezaji kufanyika Rukwa Juni

506ff866d92c46e820f169316074f877.png Kongamano la uwekezaji kufanyika Rukwa Juni

Sat, 6 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKOA wa Rukwa unatarajiwa kuandaa Kongamano la Uwekezaji la siku tatu litakalofanyika mjini Sumbawanga Juni mwaka huu.

Hayo yalibainishwa na Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa, Bernard Makali alipowasilisha taarifa ya maandalizi ya Kongamano la Uwekezaji katika Kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Rukwa (RCC) kilichofanyika mjini hapa hivi karibuni.

“Kongamano hilo litajumuisha uzinduzi rasmi wa Kitabu cha Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Rukwa, maonesho yatakayofanyika viwanja vya Ndua na wadau na wawekezaji kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio,” alieleza Makali.

Makali alisema wageni 350 wataalikwa kuhudhuria kongamano hilo na Sh 133,550,000 zinahitajika kuliandaa.

“Kila halmashauri imeagizwa kuchangia shilingi 33,387,000, zipo halmashauri nne, Manispaa ya Sumbawanga na halmashauri za wilaya za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo,”alifafanua.

Alisema wafanyabiashara wa hoteli zote mkoani Rukwa, wamehamasishwa kuanza kuziboresha ikiwemo kuzipaka rangi, kuhakikisha maji yapo wakati wote na kuhakikisha barabara zinazoenda kwenye hoteli hizo zinakarabatiwa.

Makali alitaja changamoto iliyopo ni uwezo wa mkoa kumudu mapokezi makubwa ya wageni 350 kwa wakati mmoja. Alisema mkoa bado hauna nyumba za kutosha za kulala wageni na pia hoteli nyingi bado hazina huduma bora kwa wageni.

Chanzo: www.habarileo.co.tz