Wananchi wa Kijiji cha Mnkonde, Kata ya Msanja wilayani Kilindi, wameomba mamlaka husika kuwaondoa wafugaji wa jamii ya Kimasai walioweka makazi kwenye Hifadhi ya Msitu wa kijiji hicho ya Mlima Mbwego.
Mwenyekiti aliyemaliza muda wake kijijini hapo, Juma Kihala, anasema walianza kupata elimu kuhusu umuhimu wa kuhifadhi misitu kupitia mradi wa FORVAC, na sasa wanaendelea na uhifadhi kupitia mradi wa kuleta Suluhisho la Ujumuishaji wa Misitu na Nishati Endelevu ya Tungamotaka Tanzania (IFBEST).
Amesema hapo awali msitu wa kijiji ulikuwa unavunwa kiholela, lakini baada ya kuanzisha ulinzi shirikishi na uvunaji endelevu, kijiji kimepata fedha zilizowezesha kukamilisha ujenzi wa zahanati, msikiti, na kisima cha maji.
Hata hivyo, anasema changamoto kubwa waliyonayo ni wafugaji wa Kabila la Kimasai kujenga makazi katika msitu wa kijiji, ingawa taratibu za kuwaondoa zimekuwa ngumu.
Mmoja wa wazee wa kijiji hicho, Zuberi Madeni, amesema uwepo wa makazi ya watu katika msitu huo umesababisha pia shughuli za ufugaji nyuki walizokuwa wakifanya katika msitu huo kutoenda vizuri, akidai kwamba mizinga inaibiwa au kuharibiwa.
Madeni amesema tatizo la wafugaji ni kuingia kijijini bila kupitia taratibu za kujitambulisha na kusaidiwa makazi na viongozi husika.
Mmoja wa viongozi wa Kamati ya Mazingira ya kijiji hicho, Zubeda Kihiyo, amesema kuwa Kijiji chao kina mpango wa matumizi bora ya ardhi, ambapo kuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya makazi na malisho, lakini wafugaji wamekuwa hawafuati utaratibu.
Waandishi wa habari walipozuru msitu huo walikuta eneo likiandaliwa kwa ajili ya kilimo na kushuhudia mabanda ya makazi zaidi ya 10.
Afisa Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira wa Halmashauri ya Kilindi, Adam Sylvester, amesema tatizo hilo wanalijua na wanalishughulikia.
Mapema, Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Hashim Mgandilwa, alipongeza mradi wa IFBEST kwa kusaidia suala la uhifadhi wa mazingira, akisema moja ya malengo ya wilaya ni kuwasaidia wafugaji wafuge kisasa kwa kuwa na ng'ombe wachache na bora.
Mradi wa IFBEST unaendeshwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA)