Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiwanda cha Tangawizi Same chaibua mvutano bungeni

E246a47281a488630edb41c106c87265 Kiwanda cha Tangawizi Same chaibua mvutano bungeni

Mon, 8 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MBUNGE wa Same Mashariki, Anne Kilango (CCM) na Mbunge wa Viti Maalumu, Naghenjwa Kaboyoka (Chadena) wamejikuta wakivutana bungeni kuhusu sakata la Kiwanda cha Tangawizi kilichopo Mamba Myamba Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Kiwanda hicho kilichoanzishwa na Kilango wakati akiwa mbunge wa jimbo hilo kabla ya Kaboyonga aliyeangushwa katika uchaguzi wa mwaka jana, kilianza kufanya vibaya kutokana na mitambo yake kushindwa kufanya vizuri na hivyo kulazimu wakulima kulipwa fidia.

Kaboyoka katika swali lake la nyongeza na msingi bungeni jana, ndiye aliyeibua mvutano huo akitaka kujua lini serikali itawalipa wakulima hao wa fedha zao, baada ya kufungiwa na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) mashine zisizo na viwango vya kuchakata tangawizi.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe wakati akijibu swali hilo alisema Ushirika wa Wakulima wa Mamba Myamba uliwapa SIDO kazi ya kutengeneza mtambo wa kuchakata tangawizi kupitia Halmashauri ya Same, unaohusisha hatua tano ambazo ni kuosha, kukata, kukausha, kusaga na kufungasha Mei 21, mwaka 2010.

“Sido iliingia mkataba na Halmashauri ya Same kwa niaba ya Chama cha Ushirika cha Msingi cha Mazao na Masoko. Aidha, Mradi huo ulikuwa na thamani ya Sh milioni 88.9,” alieleza.

Alisema mtambo huo ulisimikwa Oktoba 29, mwaka 2012 na ulifanya kazi na baadaye ukawa na changamoto. Marekebisho ya changamoto hizo yalifanyika na mtambo mwingine mpya ukasimikwa Februari 27, mwaka 2015.

Naibu waziri huyo alieleza kuwa Sido ilinunua tangawizi kwa wakulima Februari 27, mwaka 2015 kwa ajili ya kufanya majaribio kabla ya kukabidhi mtambo kwa Ushirika huo.

“Kwa sasa mtambo huo unafanya kazi vizuri na wanaushirika wanaendelea na shughuli za uchakataji wa zao la tangawizi,”alisisitiza.

Aidha, alisema Sido imeendelea kutengeneza mashine za kukatakata na kusaga tangawizi pamoja na makaushio na imeuza kwa wajasiriamali wa Same, Tanga na Dar es Salaam na zinafanya kazi vizuri.

Alisema kwa mujibu wa mkataba, majukumu ya Sido yalikuwa ni kutengeneza na kufunga mtambo kazi ambayo ilikamilika.

“Hata hivyo, serikali imeielekeza shirika hilo lishauriane na Halmashauri ya Same pamoja na Ushirika wa Mamba Myamba ili kutathmini na kukubaliana namna bora ya kutatua changamoto hiyo,” alisema.

Baada ya jibu hilo, katika swali lake la nyongeza Kaboyoka alidai kuwa jibu hilo haliendani na swali lake na kutaka ufafanuzi zaidi jambo ambalo lilimuinua Kilango, ambaye alitaka suala la kiwanda cha tangawizi aachiwe yeye aliyekianzisha, Halmashauri ya Same na Shirika la Pensheni ya Watumishi wa Umma (PSSSF).

Alisema PSSSF kwa sasa wameingia mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Same kusimika mitambo mipya.

Chanzo: habarileo.co.tz