Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kivuko chazama Ukerewe, mamia wahofiwa kufariki

Sat, 22 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Mwanza. Vilio, majonzi na simanzi vimetawala jijini Mwanza baada ya kivuko cha MV Nyerere kuzama katika Ziwa Victoria mita 50 kabla ya kutia nanga huku abiria 37 waliokuwa kwenye kivuko hicho wakifariki dunia hadi zoezi la uokoaji lilipositishwa.

Kivuko hicho kilichokuwa kikitokea katika Kisiwa cha Bugolora kuelekea Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe, kinadaiwa kilikuwa kimepakia zaidi ya abiria 100, wengi wakiwa wanaelekea kwenye gulio kilizama saa 8:05 mchana.

Soma zaidi: Kivuko chazama Ukerewe, mamia wahofiwa kufariki

Taarifa za kuzama kivuko hicho zilizokumbusha tukio la kuzama kwa meli ya MV Bukoba Mei 21, 1996 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 800, zilitolewa kwa nyakati tofauti na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, George Nyamaha.

Taarifa za viongozi hao kuhusu waliookolewa na waliopoteza maisha zilikuwa zikipishana kadri muda ulivyokuwa ukienda na timu ya uokoaji chini ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kuendelea na uokozi.

Jana saa 12 jioni, Shanna alisema kuwa watu watano walikuwa wamefariki dunia na wengine 32 kuokolewa baada ya kivuko hicho kuzama upande mmoja, kabla ya kufika kwenye Ghati ya Ukara.

Alisema, “Hiki kivuko inaelekea kina idadi kubwa ya watu walioko ndani, huenda wameshafariki dunia, ingawa uokoaji bado ulikuwa unaendelea. Vyombo mbalimbali vya usalama vipo na timu za uokoaji tayari imefika eneo la tukio na inaendelea na uokoaji,” alisema Shanna.

Kuhusu chanzo cha ajali hiyo na tani za mizigo iliyokuwamo ndani ya kivuko hicho, Shanna alisema hawezi kujua na kwamba taarifa zitatolewa baada ya zoezi la uokoaji kukamilika.

Hata hivyo, Nyamaha alisema kivuko hicho kilikuwa kimepakia tani nyingi za mizigo na kilibeba idadi kubwa ya watu tofauti na uwezo wake.

“Kivuko kilipinduka na kikageukia kilipokuwa kinatoka na kujifunika hali iliyosababisha kuwafunika watu wengi,” alisema.

Mwenyekiti huyo wa halmashauri alisema ilipofika saa 11:45 jioni, waokoaji walitumia mitumbwi wakati wakisubiri meli iliyokuwa ikitokea Mwanza mjini. Alisema wakati huo kivuko hicho kilikuwa kimezama upande mmoja na chini kulikuwa na watu.

Taarifa za awali zilieleza kuwa kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba abiria 100, tani 25 za mizigo na magari madogo matatu kilizidisha mizigo likiwamo lori kubwa la mahindi.

Kivuko hicho kilifungwa injini mpya Julai mwaka huu baada ya awali kupata hitilafu na kimekuwa kikitoa huduma kutoka Kisiwa cha Bugolora –Ukara wilayani Ukerewe tangu mwaka 2004.

Jana saa 12 jioni, meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Hassan Karonda alisema wanaendelea na juhudi na uokoaji, kwamba taarifa za kivuko hicho zitatolewa baada ya kukamilisha zoezi hilo.

Mmoja wa shuhuda wa tukio hilo, Denis Kwesiga alisema kivuko hicho kilikuwa kimepakia magari mawili likiwamo la mizigo lililokuwa limesheheni magunia ya mahindi.

Alisema kivuko hicho kimekuwa kikizidisha mizigo na abiria siku za Alhamisi kutokana na gulio hilo la Ukara.

Soma zaidi: Rais Magufuli atuma salamu za rambirambi za ajali kivuko, 37 wafariki dunia

Waliothibitishwa kupoteza maisha

Jana, saa 3:20 usiku, Kamanda Shanna alisema kwamba hadi wakati kazi ya uokoaji ikisitishwa jioni, miili iliyokuwa imeopolewa ni 37 kati ya abiria zaidi ya 100.

Kuhusu idadi kamili ya abiria, Nyamaha alisema, “Kuna maelezo kuwa katika kivuko hicho kulikuwa na abiria zaidi ya 100 baada ya kupinduka idadi kubwa ya watu wanahofiwa kufariki dunia.”

Imeandikwa na Ngollo John (Mwanza), Jovither Kaijage (Ukerewe), Asna Kaniki na Emmanuel Mtengwa (Dar)

Chanzo: mwananchi.co.tz