Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kivuko cha MV Chato kuanza kazi

1c6d199332d363c59c93bc1efa14223a Kivuko cha MV Chato kuanza kazi

Thu, 17 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya amesema kuwa ujenzi wa kivuko cha MV Chato II “Hapa Kazi Tu” umekamilika kwa asilimia 99 na kinatarajiwa kuanza kutoa huduma kati ya Chato na Nkome katika Ziwa Victoria.

Kasekenya alisema hayo mkoani Mwanza baada ya kukagua ujenzi wa kivuko hicho ambao ulianza Februari mwaka huu na umegharimu Sh bilioni 3.1. Alisema ameridhishwa na ujenzi huo.

“Kivuko kimekamilika na kimefungwa vifaa vya kisasa na vinavyoendana na wakati, hivyo natoa rai kwa wananchi kutumia kivuko hiki kwani kina usalama wa kutosha,” alisisitiza.

Aidha, naibu waziri huyo alitoa siku tatu kwa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na Chuo Cha Bahari Dar es Saalaam (DMI) kuhakikisha wanakagua kivuko hicho na kutoa vibali ili kianze kutoa huduma.

Mkandarasi wa kivuko hicho, Major Songoro, aliishukuru serikali kwa kuipa kazi kampuni hiyo na hivyo kuwajengea uwezo mkubwa katika ujenzi wa vivuko na meli nyingi hapa nchini, kwa ajili ya kuboresha huduma za usafiri kwa wakazi wa maziwa makuu.

Meneja wa Wakala wa Umeme na Ufundi (Temesa) Mkoa wa Mwanza, Karonda Hassani, alisema kuwa kivuko hicho kina uwezo wa kuchukua abiria 200, magari 10 na mzigo wa tani 100 kwa wakati mmoja.

Naibu waziri alifanya ziara ya kikazi katika mikoa ya Mwanza na Singida kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa miradi inayoendelea na ile iliyopo katika hatua za awali za ujenzi ya sekta hizo.

Chanzo: habarileo.co.tz