Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiu ya sigara yamnusuru na kifo mgodi ulioua 22

Anusurika Mgodi Pic Kiu ya sigara yamnusuru na kifo mgodi ulioua 22

Fri, 19 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati watalaamu wa afya wakionya kuwa uvutaji sigara ni hatari kwa afya za binadamu, hali imekuwa tofauti kwa Mihayo Ngalita ambaye kiburudisho hicho kimemuepusha na mauti katika mgodi aliokuwa akifanyia kazi kuporomoka na kuua waliokuwamo.

Katika tukio hilo lililotokea alfajiri ya kuamkia Januari 13, mwaka huu, wachimbaji wadogo 22 walifariki dunia kwa kuporomokewa na gema katika mgodi wa madini ya dhahabu ulioko Kijiji cha Ikinabushu Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.

Akizungumzia ajali hiyo leo, Alhamisi Januari 18, 2024 Ngalita amesema, “ni kudra na mapenzi ya Mwenyezi Mungu mimi kuwa hai hadi leo.”

Alivyonusurika

“Hamu ya kuvuta sigara ndiyo imeninusuru na kifo. Nilikuwa chini ya mgodi na wenzangu tukiendelea na kazi na tulishafikia eneo la uzalishaji kwenye mwamba wenye madini. Ghafla nilipata hamu ya kuvuta sigara na kwa bahati mbaya sikuwa na sigara kule chini,’’ anaanza kusimulia.

Anasema baada ya kupata hamu ya kuvuta sigara, alitafuta mtu wa kumtuma kwenda kumnununulia bidhaa hiyo bila mafanikio na hivyo akaamua atoke mwenyewe mgodini kwenda kununua.

Mchimbaji huyo ambaye ndiye alikuwa mlinzi wa mwamba wa dhahabu akiwasimamia wenzake mgodini anasema baada ya kununua sigara, aliamua kuvuta akiwa nje kabla ya kuanza safari ya kurejea tena ndani ya mgodi.

“Nikitumia kamba kushuka chini, nilifanikiwa kufika hadi jirani na eneo la uzalishaji nilikowaacha wenzangu; lakini ghafla gema likaporomoka na kuwafunika wenzangu ambao tayari nilishawakaribia,’’ anasema Mihayo.

Kutokana na kuwa mbali kidogo na walipokuwepo wenzake, mchungaji huyo anasema gema lililoanguka lilimfunika hadi usawa wa juu ya goti na hivyo kunasa na akishindwa kwenda mbele wala kurudi nyuma hadi alipookolewa na wachimbaji wengine waliokuwa wanaingia ndani ya mgodi.

Alipoulizwa kama waliofia mgodini waliingia kinyemela, Ngalita amekanusha, akipinga maelezo ya uongozi wa mgodi.

“Hapana! Hatukuingia kinyemela wala kuvamia mgodi. Wote tuliingia kwa kufuata taratibu ikiwemo kuandikishwa majina kabla ya kuingia ndani ya mgodi na ndiyo maana ilikuwa rahisi kuwatambua marehemu wote.

“Mchana kabla ya ajali ya usiku, wakaguzi kutoka Ofisi ya Madini walifika mgodini na kuagiza shughuli zisitishwe baada ya kubaini usalama mdogo mgodini na kweli kazi ilisimamia. Lakini ilipofika usiku tuliitwa, tukaandikishwa majina na kuambiwa tuingie tukachimbe kuongeza viroba vya mchana wa madini ili tugawane siku inayofuata,’’ anasema.

Akifafanua, mchimbaji huo anasema, “kwa mujibu wa maelekezo ya Ofisi ya Madini Mkoa wa Simiyu, siku inayofuata (Januari 13, 2024) ilipaswa kuwa siku ya mgawo wa mchanga wa dhahabu, sasa tulitaka kuongeza viroba vyenye mawe (madini) ya dhahabu ndio maana tukaambiwa tuingie kuchimba.’’

Anasema hadi gema linaanguka na kusababisha vifo vya wenzake, yeye alishachimba na kujaza zaidi ya viroba 20 vya mchanga wa dhahabu.

“Eneno lile lilikuwa na mwamba wenye madini mengi yanayoonekana kwa macho…na licha ya hatari iliyokuwa inaonekana, bado tulikuwa tayari kuingia. Hakuna mchimbaji anayeogopa kifo mgodini kwa sababu haya ndiyo maisha yetu,’’ anasema Mihayo akijibu kwa nini waliingia mgodini licha ya kuzuiwa kutokana na hatari iliyobainika.

Kauli ya Mihayo kuwa walioingia mgodini siku hiyo hawakuvamia wala kuingia kinyemela imeungwa mkono na mchimbaj mwingine aliyezungumza kwa sharti la kuhifadhiwa jina, ambaye pia anassitiza kuwa uongozi wa mgodi ulitoa baraka za kazi kuendelea.

“Mimi nilikuwepo wakati wale wachimbaji waliofariki wanaingia mgodini, wote walitafutwa na wasimamizi wa mgodi na kuwaelekeza waingie kuchimba madini,” anasema mchimbaji huyo ambaye ni miongoni mwa wamiliki wa miduara (mashimo) ya dhahabu eneo hilo.

Anasema kazi ya kuwatafuta wachimbaji wa kuingia mgodini ilianza saa 4:00 usiku na ilipofika saa 7:30 usiku wakaanza kuingia mgodini ambako walifanya kazi hadi alfajiri gema lilipowaporomekea na kusababisha vifo vya watu 22.

“Tunaogopa kujitokeza kusema ukweli viongozi wanapofika hapa kuhofia usalama na maisha yetu…lakini tukihakikishiwa usalama tutaeleza ukweli wote jinsi viongozi wa mgodi walivyoshiriki kuingiza watu ndani ya mgodi licha ya kuagizwa kusitisha kazi,’’ anasema mchimbaji huyo.

Huku akionyesha msisitizo, mchimbaji huyo anasema; “Baada ya Ofisa Madini Mkoa kuzuia shughuli zisiendelee, ni wakaguzi wa mgodi ndio walitumia njia za panya kuwaingiza baadhi ya wachimba kutokana na eneo walilofikia kuwa na mwamba wenye dhahabu nyingi,’’

Uongozi wa mgodi

Hata hivyo, uongozi wa mgodi wa Ikinabushu umeendelea kusisitiza kuwa wachimbaji walioingia mgodini waliingia kinyemelea baada ya kuwazidi ujanja walinzi waliokuwepo.

Akijibu hoja na madai ya wachimbaji kuwa uongozi ndio uliruhusu na kuratibu wachimbaji walioingia mgodini, Mkaguzi Mkuu mgodi wa Ikinabushu, Samweli Mwita anasema kabla ya maafa hayo, kundi jingine la wachimbaji lilivamia mgodi huo lakini uongozi ukafanikiwa kulidhibiti.

“Kwenye hii migodi kuna watu wanaitwa ‘Manyani’ hawa kazi yao ni kuvamia mashimo na kuchimba. Hicho ndicho kilichotokea,’’ anasema Chacha.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Mwenyekiti wa mgodi wa Ikinabushu, Masumbuko Jumanne akisisitiza kuwa uongozi ulisitisha kazi zote kutii agizo la Ofisi ya Madini Mkoa wa Simiyu baada ya ukaguzi uliobaini hali hafifu kiusalama katika migodi ya eneo hilo.

“Ofisa Madini alifika hapa siku moja kabla ya ajali na kutuagiza kusitisha shughuli ya kuchimba kwa sababu aligundua hatari kiusalama kwenye miduara…uongozi ulitii na kusitisha shughuli zote,’’ anasema Masumbuko.

Utekelezaji agizo la Wizara

Katika hatua nyingine, uongozi wa mgodi wa dhahabu wa Ikinabushu, Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu umeanza kutekeleza maagizo ya Serikali ikiwemo kuunda kikundi kitakachopewa leseni ya kuchimba madini eneo hilo.

Baada ya kuundwa, kusajiliwa na kupewa leseni, uongozi wa kikundi hicho ndio utapewa masharti ya kutekeleza kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu kabla shughuli za uchimbaji kuruhusiwa kurejea tena mgodini hapo.

Maagizo hayo yalitolewa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde Januari 14, 2024, baada ya kutembelea mgodi huo ulioua wachimbaji 22 baada ya kuangukiwa na gema wakiwa mgodini alfajiri ya Januari 13, 2024.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu juzi, Mwenyekiti wa Mgodi wa Ikinabushu, Masumbuko Jumanne amesema tayari wameunda kikundi cha  Ikinabushu Goldmine Company Ltd na kuwasilisha nyaraka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bariadi kwa hatua nyingine kwa mujibu wa sheria.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga amethibitisha kupokea nyaraka zinazohusiana na kikundi cha Ikinabushu Goldmine Company Ltd, ambacho hata hivyo amesema bado hakijakidhi vigezo na masharti ya usajili na wahusika wameelekezwa maeneo ya kurekebisha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live