Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kituo cha utalii kunufaisha wanawake jamii ya Kibarbeig

82753 Pic+utalii Kituo cha utalii kunufaisha wanawake jamii ya Kibarbeig

Mon, 4 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Babati. Wanawake wa jamii ya Kibarbeig wanaoishi eneo la Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori Burunge (JUHIBU), wataanza kunufaika na utalii baada ya kujengewa kituo cha kitamaduni watakachokitumia kuonyesha na kuuza vifaa vya kitamaduni kwa watalii.

Ofisa Utamaduni wa wilaya ya Babati, Beatrice Maliseli  akizungumza katika uzinduzi wa kituo hicho Leo Jumapili Novemba 3, 2019, aliwataka wanawake wa jamii hiyo kukitumia  vizuri kujiongezea kipato.

Amesema sasa watalii wataweza kuwatembelea na kununua vifaa vyao , kuona ngoma na tamaduni zao na hivyo kujiongezea fedha kwa ajili ya maisha yao.

Maliseli aliwataka wanawake na vijana wa jamii hiyo,kuongeza ubunifu wa vifaa vyao na kuanza kujifunza lugha za kigeni ili waweze kuwasiliana vizuri na watalii.

Ofisa maendeleo ya jamii kutoka taasisi ya Chemchem, Walter Pallangyo amesema taasisi hiyo imeamua kuwajengea jamii hiyo kituo hicho ili kuweza kunufaika zaidi na Utalii.

“Watalii ambao watakuja katika maeneo tuliowekeza tutawaleta hapa pia kuona Utamaduni wenu na kununua vifaa vyenu,” amesema. Mtalii kutoka nchini Uholanzi, Jan Neggers akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea kituo hicho na kununua bidhaa za jamii hiyo, amesema ni mara yake ya kwanza kushuhudia tamaduni za jamii hiyo ya Kibarbeig na wamefurahi.

“Familia yangu imefurahi kutembelea kituo hiki kwani pia tumejifunza maisha ya jamii hii ya asili na tukirudi nyumbani tutakuwa mabalozi wao wazuri,” amesema.

Kiongozi wa mila wa jamii hiyo, Garimi Mebati amesema wamepata kituo hicho Kwa wakati muafaka  kwani kwa miaka mingi wamekuwa na mgogoro uliotengenezwa katika kijiji hicho na hivyo kushindwa kupata fursa za kunufaika na utalii.

Mebati anasema wanaishukuru Serikali kuendelea kutatua kero zao.

Chanzo: mwananchi.co.tz