KITUO kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Mbezi Luis, Dar es Salaam kinatarajiwa kuanza kutumika Alhamisi wiki hii.
Mkuu wa Mkoa huo, Abubakar Kunenge , alisema jana kuwa, kuanza kutumika kwa kituo hicho ni mwanzo wa kufungwa rasmi kwa kituo cha mabasi cha Ubungo (UBT).
Kunenge aliwaeleza waandishi wa habari kituoni hapo kuwa, maandalizi kwa ajili ya kukiwezesha kituo hicho kutoa huduma yamekamilika.
"Tunaomba ujumbe muhimu uwafikie wamiliki wote wenye mabasi kuwa siku hiyo rasmi shughuli zao za utoaji wa huduma zitaanza kufanyika katika kituo hiki kipya" alisema.
Kunenge alisema, ni muhimu wasafirishaji na wadau wengine wa kituo hicho kipya wahakikishe wanafanya maandalizi ya kutosha katika siku chache zilizobaki ili kujiepusha na changamoto zinazoweza kujitokeza.
Alisema changamoto ya barabara ya kuingia kituoni hapo imetatuliwa baada ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuijenga hadi eneo la kituo hicho.
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana, alisema tayari uongozi wa jiji hilo umeweka utaratibu kuwawezesha wafanyabiashara ndogondogo wafanye shughuli zao bila bughudha.
Liana alisema, kwa kuanzia uongozi wa jiji umejenga mabanda ya muda pembeni ya kituo wakati ujenzi wa eneo la kudumu ukiendelea ukihusisha huduma za msingi vikiwemo vyoo, bafu na nyinginezo.
Alisema, kwa upande wa watoa huduma za biashara , uongozi wa jiji hilo imeweka utaratibu utakaotumika kuwaingiza katika kituo hicho ukiondoa wafanyabiashara wenye madeni katika kituo cha mabasi cha Ubungo.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, aliwahakikishia usalama abiria na watumiaji wa kituo hicho, na akawataka wapigadebe katika kituo cha Ubungo wasisogee kwenye kituo kipya.
Kamanda Mambosasa alisema, kituo kitakapoanza kazi, mwisho wa wapigadebe uwe katika barabara za mzunguko Ubungo, na kwamba, na wakithubutu kufika kwenye kituo kipya watakumbana na mkono wa sheria.
Alisema Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kusimamia usalama katika kituo hicho kwa kuweka askari wa kutosha muda wote.
Ujenzi wa kituo cha mabasi cha Mbezi Luis ulianza miaka miwili iliyopita ukiigharimu serikali zaidi ya Sh bilioni 50 na kinatarajiwa kuhudumia mabasi takribani 300 kwa siku.