Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kituo cha kupozea umeme Bulyanhulu chakamilika

27c27eae1f4906dc37a24fd3553a7af2 Kituo cha kupozea umeme Bulyanhulu chakamilika

Sat, 9 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Nishati, Dk Medard Kalemani amesema kuwa kituo kidogo cha kupokea na kusafi risha umeme kwenda mkoani Geita na Nyakanazi hadi Kigoma, kilichopo Bulyanhulu wilayani Kahama mkoani Shinyanga kilichogharimu Sh bilioni 55 kimekamilika kwa asilimia 100.

Aliyasema hayo jana alipotembelea kituo hicho, kilichoanza kujengwa mwezi Septemba na kukamilika mwezi Novemba mwaka jana.

“Serikali tuliona kituo hiki kipanuliwe ili kuongeza nguvu kwa kusafirisha nishati ya umeme kwenda mkoani Geita, kuongeza nguvu mkoani Mwanza na Nyakanazi hadi Kigoma, wataalamu walisema hawawezi ardhi ni ngumu lakini walijitahidi wakaweza kwa kipindi kifupi na kimekamilika kwa asilimia 100 na kuanza kazi,” alisema.

Dk Kalemani alisema kuwa mradi huo ni wa muhimu, kwani utakwenda takribani kilomita 44 Geita hadi Nyagh’wale na Nyakanazi hadi Kigoma kilomita 94. Mradi huo utatumia gridi ya taifa na utasambaza pia umeme katika vijiji 39 vilivyopitiwa na njia kuu.

Alisema kuwa mpaka sasa kuna vijiji 32 vimepitiwa na umeme huo. Alisema mahitaji ya umeme kwa wananchi ni makubwa. Dk Kalemani aliwataka watumishi wa Tanesco wafyeke miti iliyopita kwenye nyaya za umeme ndani ya siku 14, kwani miti inasababisha umeme kukatika hovyo.

Msimamizi wa Kituo cha Bulyanhulu, Amos Asheli alisema kulikuwa na changamoto ya kukosekana kwa umeme mara kwa mara kabla ya mradi huo. Lakini, alisema hivi sasa umeme upo wa kutosha kuanzia wilaya ya Kahama hadi mkoa wa Geita .

Mbunge wa Msalala, Idd Kassim alisema kuwa mradi huo wataulinda mradi huo. Alisema kituo hicho kipo Kijiji cha Namba Tisa lakini wananchi wake hawana nishati ya umeme, hivyo alimuomba waziri Kalemani alifanyie kazi ombi hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Annamringi Macha alisema kuwa wilaya yake ina upungufu mkubwa wa umeme, hivyo kituo hicho kitawapatia umeme wa ziada.

Alisema mara nyingi wamekuwa wakitumia umeme unaotoka Kituo cha Mgodi wa Buzwagi ambao hautoshi, kwani Kahama kuna watu ni wengi.

Chanzo: habarileo.co.tz