Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kitendawili upatikanaji huduma ya maji

MAJII Kitendawili upatikanaji huduma ya maji

Mon, 28 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), ikitangaza hali ya upatikanaji wa maji kwa sasa ni asilimia 100, baadhi ya wakazi wa maeneo mbalimbali wa jiji hilo bado wameendelea kulalamikia kukosa maji.

Mgawo wa maji katika jiji hilo ulitangazwa Oktoba 25, 2022 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Amos Makalla baada ya kutembelea mto Ruvu na kukuta kina cha maji kimepungua kupita kiasi hali iliyosababishwa na ukame.

Mwezi mmoja baadaye kwa maana ya Novemba 25, 2025, mara baada ya kutembelea tena mto Ruvu na kujionea hali ilivyo, RC Makalla alitangaza kumalizika kwa mgawo huo kwa sababu ya kuongezeka kwa kina cha maji kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa jiji hilo wamedai licha ya taarifa zinazotolewa na Serikali na Dawasa kuonyesha matumaini bado hawana uhakika wa maji kupata maji safi na salama kwenye maeneo yao.

Kupitia ukurasa wa Instagram wa Mwananchi, Said Mintange ambaye ni mkazi wa Goba amesema eneo hilo halina maji ya Dawasa hivyo wamekuwa wakitegemea maji ya visima pekee.

Maoni kama hayo yalitolewa na Rita Farhan, mkazi wa Tabata Chang’ombe aliyeeleza kwenye eneo lao takribani wiki nzima hawajapata maji.

Naye Marcel Ivambi mkazi wa Mbezi Msakuzi alieleza kukosekana kwa maji kwenye mitaa yao na kuziomba mamlaka husika ziwafikishie huduma hiyo muhimu.

Leo Jumatatu, Novemba 28, 2022, akizungumza na waandishi wa habari, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja ameeleza maji yanapatikana kwa asilimia 100 na hali hiyo imesababishwa na kuongezeka kwa uzalishaji wa maji kutoka chanzo cha mto Ruvu kutoka lita 300 milioni katika kipindi hicho cha mgano hadi lita 520 milioni ambazo huzalishwa kwa kawaida.

Mhandisi Luhemeja amesema kiwango hicho kinaungana na lita milioni 70 zinazozalishwa katika mradi wa visiwa wa Kigamboni na kufanya uzalishaji wa maji kuwa lita milioni 590.

Amesema hali hiyo inaondoa kabisa mgao uliodumu kwa miezi miwili huku wakiendelea kutekeleza miradi inayolenga kumaliza kabisa adha ya maji katika maeneo yenye changamoto.

Akitoa mchanganuo wa upatikanaji wa maji kwa majimbo ya jiji hilo Luhemeja amesema Kigamboni yanapatikana kwa asilimia 100 sawa na Ilala ambayo ina faida ya kupata maji kutoka mradi wa Kigamboni na Ruvu chini.

Kama ilivyo kwa Ilala, jimbo la Temeke pia limenufaika na maji kutoka Kigamboni matarajio yakiwa visima vinne vinavyoendelezwa vitazalisha maji lita milioni 28 ambayo yote yatapelekwa huko.

“Jimbo la Ubungo upatikanaji wa maji ni asilimia 100 isipokuwa hawa wana changamoto ya mfumo wa majitaka lakini sio changamoto ya ukosefu wa majisafi na salama.

“Kawe maji yanapatikana kwa asilimia 70 hadi 90 kuna mradi ambao umekamilika kufikia Ijumaa utaanza kufanya kazi na upatikanaji wa maji utakuwa asilimia 100,” amesema Mhandisi Luhemaja.

Kulingana na ofisa mtendaji mkuu huyo jimbo lenye changamoto ni Kibamba ambalo upatikanaji wake wa maji ni kati ya asilimia 60 hadi 80 sababu kubwa ikiwa ni miinuko.

Hata hivyo amebainisha kupitia mradi wa maji wa mshikamano changamoto hiyo itapatiwa ufumbuzi na tayari pampu mbili za kuvuta maji zimeshanunuliwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live