Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kitendawili chanzo moto uliozuka Mwanza hotel

Moto Kudhibitiwa Iiii Kitendawili chanzo moto uliozuka Mwanza hotel

Thu, 1 Sep 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amesema kuwa moto uliozuka na kuunguza Club Dallas iliyoko ndani ya Mwanza Hoteli umedhibitiwa huku akisema hadi sasa chanzo cha moto huo hakijafahamika.

Moto huo ulianza ya jana Jumatano usiku saa 1:14 kisha kusambaa katika eneo lingine la jengo ilipo klabu hiyo huku maofisa wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji wakiendelea upozaji wa mabaki ya moto huo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo hilo, Malima ametoa salamu za pole kwa mmiliki wa hoteli hiyo na wamiliki Club Dallas huku akisisitiza wakazi wa mkoa huo kujenga miundombinu ya kukabiliana na majanga ikiwemo moto kwenye maeneo yao.

"Tukio hili linatokea nikiwa katika eneo hili natoka ofisini nikawa naona moshi, kama unavyojua moshi hauchelewi kuwa moto. Hapa tuna ofisi nyingi za umma ikiwemo benki ya NMB na jengo la Benki Kuu, lakini moto huu umedhibitiwa," amesema Malima

Malima ameongeza; "Kama tumejifunza jambo ni kwamba kwenye majanga kama haya hakuna cha kusema tulidhani tunatakiwa kuwa tayari wakati wote,"

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Kamila Labani amesema uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha moto huo huku akisisitiza kwamba hakuna madhara kwa binadamu badala yake wanaendelea na utambuzi wa mali zilizoteketea katokana na moto huo.

Laban amesema kudhibitiwa kwa huo ni matokeo ya kuunganisha nguvu kati ya magari ya zimamoto kutoka Kiwanda cha Nile Perch, Uwanja wa Ndege, Mwauwasa, JWTZ na magari ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani hapa.

"Ukiwa na vitu vya plastiki ndani kunasababisha moto usambae kwa haraka sana lakini tumepambana kwa nguvu zote tumefanikiwa kuudhibiti kwa kasi na nguvu kubwa sana," amesema Labani

Amewaomba wamiliki wa majengo kuhakikisha majengo yao yana mifumo ya maji inayoweza kusaidia kidhibiti moto unapoibuka kwa dharura huku akidokeza kwamba moto uliozuka katika hoteli hiyo umefanikiwa kudhibitiwa kutokana na mifumo iliyoko kwenye Jengo la Benki Kuu mkoani Mwanza kufanya kazi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana amewataka wamiliki wa hoteli hiyo kuwa watulivu wakati huu ambao wamekumbwa na tukio la kuunguliwa na hoteli hiyo.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz