Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kishapu wapitisha bajeti Sh39.4 bilioni kwa 2023/24

Kishapu Pic Kishapu wapitisha bajeti Sh39.4 bilioni kwa 2023/24

Sat, 21 Jan 2023 Chanzo: Mwananchi

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Kishapu mkoani Shinyanga limejadili na kupitisha mpango wa bajeti wa mwaka 2023/2024 wenye jumla ya Sh39.4 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo.

Kwa mujibu wa taarifa ya bajeti hiyo, mishahara (PE) ni zaidi ya Sh23.73 bilioni na maendeleo ni zaidi ya Sh10.32 bilioni.

Taarifa hiyo pia inaonyesha mapato ya ndani yasiyofungwa ni Sh3.9 bilioni, mapato yaliyofungwa ni zaidi ya Sh940.68 bilioni na ruzuku ya matumizi mengineyo (OC) ni zaidi ya Sh882.59 bilioni.

Wakijadili bajeti hiyo jana Januari 20, baadhi ya Madiwani wa halmashauri hiyo, wamesema itatumika kutekeleza kipaumbele cha halmashauri cha kukamilisha viporo vya miradi ya maendeleo iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi.

Diwani wa kata ya Seke, Bugoro Mpogomi amesema bajeti hiyo waliyoipitisha wanatakiwa wakaisimamie ipasavyo.

"Bajeti yetu tumeipitisha leo, tunasisitiza wakuu wa idara na sisi wenyewe madiwani twendeni tukazisimamie kikamilifu fedha zetu tulizozipitisha wenyewe kwa ajili ya maendeleo ya halmashauri yetu na zikatatue changamoto za watu wetu ili kuhakikisha kero zilizopo zinaisha," amesema Mpogomi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, William Jijimya ambaye ni Diwani wa Kata ya Mondo ameagiza bajeti hiyo ikasimamiwe na kuheshimiwa.

"Bajeti hii imepitishwa kwa makusudi watumishi na madiwani simamieni ipasavyo lengo la Serikali ni kuona mapato yanasimamiwa kwa asilimia 100,” amesema.

Naye Katibu tawala wa Wilaya ya Kishapu, Shadrack Kengese bajeti hii iliyopitishwa leo ikasimamiwe na miradi ya mkakati iliyopo ikasimamiwe na kukamilishwa kwa wakati ikiwa ni pamoja na mapato ya ndani yakafikiwe, ili wilaya ya Kishapu ikawe ya mfano.

Aidha mkurugenzi wa halmashauri hiyo Johnson Emmanuel amesema bajeti hiyo iliyopitishwa wataisimamia ipasavyo ili kuhakikisha inatekeleza miradi ya maendeleo.

Chanzo: Mwananchi