MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Ilemela,kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk Angelina Mabula amewaahidi wakazi wa kata ya Kirumba kuwa atahakikisha anatatua kero ya maji haswa kwa wanaoishi katika maeneo ya mlimani.
Dk Mabula aliahidi hayo wakati alipokuwa kwenye mkutano wa kampeni katika viwanja vya kanisa la Sabato. Dk Mabula alisema wakazi ya mtaa wa mlimani A na B wanakabiliwa na kero hiyo.
Alisema tayari Serikali ilitengea bilioni 7.7/- kwajili ya utatuzi na ujenzi wa miundo mbinu ya maji katika wilaya ya Ilemela. Aliahidi pia ujenzi wa soko kuu kubwa na kisasa katika kata ya Kirumba ambapo tayari Serikali imetenga shilingi bilioni 13/-
Dk Mabula alisema watajenga matenki ya Maji katika maeneo ya Kitangiri na Mji Mwema.Katika sekta ya Elimu, Mabula alisema wamewekeza shilingi milioni 72 kwajili ya ujenzi wa maabara na madarasa katika shule za sekondari Kabuhoro na Kirumba.
Alisema katika urasimishaji wa Ardhi, jumla ya wakazi 602 wamechukua hati huku katika mtaa wa Kilimani ni wakazi 35 na mtaa wa Kabohoro ni wakazi 430.
Kwa upande wake mgombea udiwani wa kata ya Kirumba kupitia CCM,Wesa Juma aliahidi kushirikiana vyema na mbunge katika kusaidia ujenzi wa kituo cha Afya katika kata ya Kirumba. Aliahidi pia kupambana na kuhakikisha ujenzi wa barabara za Kirumba na kilimani.