Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Abdalla Shaibu Kaim amewataka viongozi wa serikali, wilayani Siha mkoani Kilimanjaro kuwabana wataalamu wa ujenzi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kwa ubora.
Kaim ametoa rai hiyo jana Juni 26, 2023 wakati Mwenge wa uhuru ulipotembelea na kuweka jiwe la msingi katika zahanati ya Naibili Kata ya Makiwaru wilayani humo, ambapo ametaka miradi isimamiwe vizuri ili kumtia moyo Rais Samia Suluhu Hassan.
"Sisi wakimbiza mwenge tunapita, lakini bado miradi inaendelea ni wajibu wenu viongizi wote kuhakikisha mnaendelea kumsimamia vizuri miradi hii ili kumtia moyo na matumaini Rais Samia Suluhu Hassan," amesema Kaim.
Amewataka viongozi kutowaamini wataalamu, ambao amesema mara nyingi husongwa na miradi mingi kiasi cha kuzidiwa.
"Nasisitiza kwenye miradi yetu tuchukue wataalamu ambao kimsingi watakuja kukagua kwenye maeneo ya nyaraka pamoja na miradi husika ili kwa kina tujiridhishe na viwango," amesema Kaim.
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo, Ezekiel Lukumay ameipongeza Serikali kwa kuwajengea zahanati hiyo iliyogharimu zaidi ya Sh278 milioni, kwani itasaidia kutoa huduma hata kata za jirani.
Naye Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Wilfred Mosi amesema ameshukuru Serikali kwa kuwaletea fedha za miradi ikiwamo ya barabara na kuahidi kutekeleza maagizo yote ya kionmgozi wa mbio za mwenge.
Zahanati hiyo ni miongoni mwa miradi saba iliyozinduliwa ikiwa na thamani ya Sh2.2 bilioni, ikiwamo pia shule ya msingi Munge iliyogharimu Sh250 milioni, inayotarajiwa kusaidia watoto wanaotoka jamii za wafugaji waliokuwa wakitembea umbali mrefu kufika shule.