Mbogwe. Wahandisi wa maji katika halmashauri mbalimbali nchini wametakiwa kutotumia kisingizio cha ufinyu wa bajeti kuacha kutibu maji kwenye visima vinavyotumiwa na wananchi.
Badala yake wametakiwa kutenga fedha kwenye mapato ya ndani na kutibu maji kwa usalama wa afya za wananchi.
Rai hiyo imetolewa leo Jumamosi Mei 4 na kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Mzee Mkongea Ali baada ya kutembelea miradi ya maji katika wilaya za Bukombe na Mbogwe na kubaini wahandisi hawatibu maji kwa madai ya halmashauri kutokuwa na fedha na wanasubiri kupewa dawa na wizara ya maji.
Amesema madhara yanayosababishwa na maji yasiyo salama ni makubwa na yanaweza kujitokeza haraka na wakati mwingine baada ya miaka kupita, hivyo kitendo cha halmashauri kutokuwa na utaratibu wa kupima na kutibu maji ni hatari kwa afya za watumia maji.
“Nyie mnachimba visima mnawakabidhi wananchi wao wakiona maji ni meupe wanajua ni salama lakini utaratibu mnaujua kila baada ya miezi mitatu mnapaswa kutibu maji wahandisi simamieni taaluma zenu, ongeeni na wakurugenzi mtenge fungu la dharura kutibu maji,” amesema Ali.
Mhandisi wa maji wilaya ya Mbogwe, Daudi Mlima amesema ufinyu wa bajeti ndiyo sababu kuu ya kutopima na kutibu maji na kwamba halmashauri hiyo haipati dawa ya“chloride” ya kutibu maji kutoka serikalini kutokana na wao kutokuwa na mamlaka ya maji.
Amesema kutokana na kukosa fedha za kutibu maji hutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuchemsha maji kabla ya kunywa.
Alisema wilaya hiyo yenye wakazi zaidi ya 193,000 ni asilimia 62 ya wananchi wake wanapata huduma ya maji na kwamba ina visima 498 na kwa utaratibu vinapaswa kupimwa na maji kutibiwa kila baada ya miezi mitatu lakini kutokana na ufinyu wa bajeti hawafanyi hivyo.
Wakati Mwenge wa Uhuru ukiacha simanzi wilayani Bukombe kwa kukataa miradi miwili ya maji, kwa wilaya ya Mbogwe imekua kicheko baada ya kuridhia miradi iliyoandaliwa yenye thamani ya Sh. 4.6 bilioni