Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kingwande: Uchaguzi ujao zamu ya wanawake

50217 Pic+kigwande

Thu, 4 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

“Ukinikuta nimebeba ndoo ya samaki natoka Feri huwezi kuamini kama mimi ni diwani.

“Udiwani kwangu ni wito wa kutumikia wananchi siioni kama ajira ya kutegemea inilipe. Nawahamasisha wananchi ninaowatumikia kuwa wajasiriamali kujiongezea kipato, ndiyo maana na mimi nafanya ujasiriamali,” anaeleza Diwani wa viti maalumu (CCM) kutoka Mkuranga, Fatma Kingwande.

Kingwande anasema aliingia kwenye ulingo wa siasa mwaka 2010 na kuwania nafasi hiyo ndani ya chama na akateuliwa. Pia, mwaka 2015 aliipata kwa mara ya pili.

Anasema ana ndoto za kuendeleza mapambano kwenye ulingo wa siasa.

“Nikiwa hai nina mpango wa kugombea kiti cha udiwani wa kuchaguliwa. Lengo langu ni kuona ninapanda na kuonyesha uwezo wangu zaidi kisiasa,” anasema Kingwande.

Kingwande anasema amepitia kipindi kigumu katika siasa lakini kutokana na kuweka mizizi na mahusiano bora na wenzake aliteuliwa tena mwaka 2015.

“Nilifiwa na mume wangu mwezi wa sita na uchaguzi unafanyika mwezi wa saba, nilipomaliza eda ndani ya siku 40, nikaanza harakati za kuwania nafasi yangu.

“Nashukuru kuishi na watu vizuri, kushirikiana na madiwani wenzangu, kutatua changamoto za wananchi zilizo ndani ya uwezo wangu, kuwasikiliza, kulia nao na kufurahi nao kulinisaidia nikateuliwa tena,” anasimulia Kingwande.

Kingwande anasema hali hiyo na mapito mengi kwenye siasa ndiyo yanampa nguvu ya kuwania udiwani kwa kuomba kura kwa wananchi.

“Nina hamasa, nimepitia hatua nyingi ngumu, familia ilinipa baraka na jamii ilinipokea, ingawa kwa wakati ule ilikuwa bado wanawake kukubalika kwenye masuala ya siasa.

“Lakini, nilikuwa na ushawishi na kila niliyekutana naye wanawake kwa wanaume niliwaaminisha uwezo wa wanawake kufanya vizuri kwenye nyanja hiyo, wakanielewa na mambo yanakwenda,” anasema.

Anasema mara nyingi wanawake wanaogopa kuingia kwenye siasa kwa kufikiria watu watasema nini kuwahusu.

“Kitu kizuri na cha kudumu huwa kinahitaji muda, akili na ubunifu, hivyo wasiogope kupoteza muda kwenye siasa, wawe wabunifu kukabiliana na waliowakuta kwa sababu hakuna anayeachia kiti chake,” anasema.

Anasema kwa sasa wanawake ndiyo wanafanya vizuri kwenye nyanja mbalimbali za uongozi, hivyo hilo liwape hamasa wanawake popote walipo kuwania nafasi za uongozi kwenye uchaguzi ujao.

Anawaasa wanawake popote walipo kuungana mkono na kuacha kukatishana tamaa.

“Unajua sisi ndiyo wapiga kura wakuu, tukiungana mkono kama tunavyofanya huku Mkuranga naamini wanawake wengi wanashinda viti wanavyowania na watateuliwa kwa wingi,” anasema.

Kingwande anawatolea mfano mawaziri kama Jenista Mhagama, waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (sera, bunge, ajira na watu wenye ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako (Elimu) na Ummy Mwalimu (Afya) namna wanavyochapa kazi na kuonyesha kuwa hakuna tofauti kati ya wanawake na wanaume katika uongozi.

“Tena nakwambia wanawake wana bidii sana ili kuuaminisha umma kuwa wanaweza kwa sababu mwanzoni huwa wanabezwa,” anasema.

Anasema mwaka 2019/2020 ni wakati wa wanawake kula sahani moja na wanaume majimboni, kwenye kata na ngazi ya taifa.

Kingwande haoni kama kuna changamoto anayopaswa kuilalamikia zaidi ya kuzitafutia ufumbuzi ziliozopo.

“Natamani wanawake wote wanaotaka kufanya siasa, iwe ngazi ya kijiji, kata, tawi, mkoa na taifa kuacha kuzungumzia changamoto.

“Badala yake wakikutana wajadili namna ya kuzitatua, hakuna atakayeacha shughuli zake kutatua changamoto za wengine kama wenyewe hamjajadili jinsi ya kuzitatua,” anasema Kingwande.



Chanzo: mwananchi.co.tz