Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kimeta chapiga hodi Moshi, RC atoa neno

43956 Pic+wasup Kimeta chapiga hodi Moshi, RC atoa neno

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Watu 97 wanahofiwa kuambukizwa ugonjwa wa kimeta, Kijiji cha Kilema wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya kusadikiwa kula nyama ya ng'ombe yenye vimelea vya ugonjwa huo.

Kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo ambao umeripotiwa siku nne zilizopita, Serikali mkoani Kilimanjaro imetoa kinga ya maambukizi ya ugonjwa huo ambao tayari umeshaua watu wawili huku wengine watano wakilazwa katika Hospitali ya Rufaa KCMC.

Akizungumza na Mwananchi leo Februari 26, 2019,  Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema hadi sasa madaktari wa mifugo na binadamu wanashirikiana kupima nyama ya ng'ombe iliyoliwa na watu hao ili kuithibitisha kitaalamu kama ina vimelea vya ugonjwa wa kimeta.

Mghwira amesema madaktari hao wanachunguza ili kubaini chanzo cha maambukizi endapo yanatoka kwa wanyamapori au kwa mifugo.

Amesema juhudi za kutambua ugonjwa huo zinafanywa na timu ya wataalamu wa ngazi ya mkoa huo na kama itabainika vinginevyo, watatoa taarifa Wizara za Afya na Mifugo ili ziweze kuingilia kati.

"Nitoe tahadhari kwa wakazi wa mkoa huu wa Kilimanjaro na maeneo mengine  ya jirani kujiepusha na kula nyama ambayo haijapimwa kitaalam," amesema Mghwira.



Chanzo: mwananchi.co.tz