Wakazi wa kitongoji cha Nyangalamila B kata ya Irenza Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema mkoani Mwanza wamemkataa diwani wa kata yao baada ya kufukia kisima walichokuwa wanachimba kwa ajili ya kupata huduma ya maji karibu.
Wakazi hao wamesema kutokana na Kitongoji hicho kukosa huduma ya maji kwa muda mrefu hali inayowapeleka kutembea zaidi ya kilometa tano kutafuta huduma hiyo na kwamba wakienda ziwani wanashambiliwa na mamba waliueleza uongozi wa Kitongoji hicho ukaamua kumueleza Mbunge wa Jimbo hilo la Buchosa, Eric Shigongo aliyetoa fedha ya kuchimba kisima hicho ili kuwaondolea adha hiyo ya kuliwa na mamba lakini cha kushangaza diwani akakifukia.
"Mbunge wetu ametuonea huruma akatuchimbia kisima lakini tunashangaa sisi wanakijiji cha Nyangalamila diwani akaja kufukia kisima anatutakia mema au mabaya?
Kwa upande wake diwani wa kata hiyo Mneke Mauna anayedaiwa kufukia kisima hicho amesema aliamuru kifukiwe kutokana na kutoutambua mradi huo kwenye eneo la kata yake.
Fikiri Dotto ni mwenyekiti wa kitongoji hicho cha Nyangalamila B akaeleza masikitiko yake baada ya diwani kufukia kisima hicho.
"Tunaomba fikisheni taarifa kwa mbunge na Rais Samia wazipate hizi taarifa kwamba Samia ametoa fedha kwa sababu ya kuwasaidia wananchi na ilani ya CCM inasema kwamba miradi ya maendeleo wananchi wasaidiwe leo mheshimiwa diwani amekuja kufukia kisima naomba mtufikishie taarifa kwa mbunge pamoja na Tanzania nzima kama kweli Tanzania nzima ina madiwani kama huyu wasiowatakiwa wanachi wao mema."