Arumeru. Vikosi vya uokoaji, vinaendelea kumtafuta Muongoza watalii, Samwel Mhina (33) pamoja na Mtumbwi aliokuwa amepanda baada ya jana jioni kuzama katika ziwa Momella kutokana na kimbunga kilichoukumba mkoa wa Arusha.
Katika tukio hilo, watalii wawili na muongoza watalii mwingine mmoja, waliokolewa baada ya Ziwa hilo kuchafuka ghafla majira ya saa nane na nusu mchana hadi saa 10 jioni.
Kamanda wa Polisi wa Oparesheni mkoa wa Arusha Francis Joseph akizungumza leo Octoba 3 wakati zoezi la kumtafuta Mhina na Mtumwi likiendelea amesema kuwa tukio la uokoaji lilianza Jana jioni bila ya mafanikio.
"Hadi leo bado tunamtafuta kijana huyu, mitumbwi iko kwenye maji kwa kuendelea kumtafuta huku wakitumia nyavu kutazama kama mwili umezama chini ya ardhi.. Jana jioni watalii wawili pamoja na muongoza watalii mmoja waliokolewa wakiwa hai"amesema.
Afisa mwandamizi wa hifadhi ya Taifa ya Arusha, Maria Kirombo amesema katika tukio hilo Mitumbwi miwili ilikuwa ikifanya utalii katika ziwa hilo, kulikuwa na watalii wawili pamoja na waongoza watalii wawili ambao ni Alpha Mosha 24 na Samweli Mhina (33).
Amesema baada ya kimbunga kuvuma, Mtumbwi uliokuwa ikiongozwa na samweli ulizama ndipo alipoanza kuogelea na kupotezana na wenzake na kuweza kupatikana yeye na wenzake watatu wakiwa hai.
Pia Soma
- Pundamilia wa ajabu ahamia Tanzania akitokea Kenya
- Diamond, Tanasha wapata mtoto wa kiume
- VIDEO: Profesa Lipumba adai demokrasia inaminywa Tanzania
Mzazi wa kijana huyo ambaye bado hajapatikana Geldat Mhina amesema kuwa taarifa ya tukio hilo aliipata akiwa katika hifadhi ya Manyara akiwa ni mfanyakazi wa hifadhi ya hiyo hivyo aliitwa ofisini na kuja katika tukio hili.
"Natarajia mtoto wangu atapatikana akiwa hai au amekufa tuendelee kumuomba mungu afanikishe katika hili" amesema
Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Jerry Muro amewapa pole familia ya Mhina amewataka wananchi kuendendele kuwa na subra kwa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinafanyakazi na kufanya jitihada ya kumpata samweli na taarifa sahihi zitatolewa .