Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilosa yajipanga kujenga sekondari 4

5a1e4c3f02af0a39e1b18242abf476fd Kilosa yajipanga kujenga sekondari 4

Mon, 8 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro imeamua kujenga shule mpya nne za sekondari ikiwemo moja maalumu kwa wanafunzi wa kike ili kuondokana na changamoto za ukosefu wa vyumba vya madarasa kila mwaka kwa wanafunzi.

Katika hatua ya awali imetenga Sh milioni 400 kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 ambazo zimeanza kutumia kwenye uboreshaji elimu ya sekondari na ujenzi wa shule mpya kwa mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Asajile Mwambambale alisema hayo juzi wakati akizunguza na HabariLEO kuhusu mikakati ya maboresho kwenye sekta ya elimu ya msingi na sekondari wilayani humo.

Mwambambale alisema ujenzi wa shule ya sekondari maalumu ya wanafunzi wa kike inayojengwa eneo la Manzese , Kilosa Mjini upo katika hatua ya msingi.

"Wilaya ya Kilosa ipo katika maandalizi makubwa ya kuona wanafunzi wanaofaulu darasa la saba wote wanaingia kuendelea na masomo ya sekondari bila kuachwa na kwa sasa waliofaulu kuingia kidato cha kwanza wapo madarasani" alisema.

Alisema kwa sasa wanakamilisha ujenzi wa madarasa mawili kwenye Shule ya Sekondari Magole , darasa moja katika Shule ya Sekondari Mikumi.

Mkurugenzi mtendaji huyo alisema ili kuondokana na uhaba wa vyumba vya madarasa kila mwaka , wilaya imeamua kujenga shule moja maalumu ya wasichana eneo la Manzese mjini Kilosa .

"Ujenzi wa shule hii kwa sasa ipo hatua ya msingi na hadi mwisho mwa mwaka huu itakuwa imekamilika na mwaka ujao wa masomo(2022) itakuwa tayari kuchukua wanafunzi wa kike wa wilaya ya Kilosa," alisema.

Alisema wilaya hiyo pia imekusudia kujenga shule nyingine tatu katika eneo la Mikumi ili kukabiliana na idadi kubwa ya wanafunzi wanaofaulu shule za msingi zilizopo kwenye tarafa ya Mikumi.

"Ujenzi wa shule hizi unatarajia kuanza Machi mwaka huu na hadi kufikia mwezi Desemba zitakuwa zimekamilika ili watakapochanguliwa wanafunzi wapya 2022 wawe wanapata masomo yao moja kwa moja " alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo alisema " lengo tusiwe na upungufu kabisa wa miundombinu ya madarasa na madawati kwa ajili ya wanafunzi wetu wote wa msingi na sekondari ...lakini kwa sasa tumeleleza nguvu shule za sekondari ili wanafunzi wetu wote wawe madarasani" alisema.

Wakati huo huo ,Manispaa ya Morogoro kwenye mwaka fedha wa 2020/201 ilitenga Sh milioni 700 na kati ya hizo Sh milioni 500 ni kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi wa shule mpya moja ya ghorofa itakayo kuwa na madarasa 25.

Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Sheilla Lukuba alisema hayo hivi karibuni mjini hapa kuwa sehemu ya fedha hizo , Sh milioni 200 zitatumika kuongeza vyumba vya madarasa kwenye shule za zamani za sekondari .

Chanzo: habarileo.co.tz