Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilio cha mtoto aliyefichwa taarifa ya vifo vya wazazi chaibua simanzi upya

84640 Mwananfunzi+pic Kilio cha mtoto aliyefichwa taarifa ya vifo vya wazazi chaibua simanzi upya

Mon, 18 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ni kawaida kwa baadhi ya makabila kulia msibani kwa kusema maneno tofauti ya kuonyesha uchungu au kupoteza matumaini baada ya kuondokewa na mpendwa wake.

Baadhi hulia kwa kumuuliza maswali mpendwa aliyefariki kana kwamba anasikia na swali moja huja baada ya jingine,

Ndivyo ilivyokuwa kwa Anna Zambi, binti wa miaka 16 aliyefichwa taarifa za vifo vya wazazi wake waliofariki wakiwa njiani kwenda kuungana naye katika mahafali ya kidato cha nne Shule ya Sekondari Mother Theresia of Calcutta, inayoendeshwa na jimbo la kanisa Katoliki Same mkoani Kilimanjaro.

“Mbona mmeniacha peke yangu? Kwanini imekuwa hivi baba na mama? Mmeondoka hamjaniachia wadogo zangu ili niwalee, nitaishije peke yangu?” Alisema Anna mara baada ya kuwasili nyumbani kwao jijini Dar es Salaam na kutaarifiwa rasmi kuhusu vifo hivyo.

Hakuna aliyestahimili kuendelea kusikiliza sauti hiyo iliyojaa maneno ya huzuni bila ya kuangua kilio.

Wazazi hao Wilfrida Lyomo na Lington Zambi na wadogo zake watatu Lulu, Grace na Andrew walipoteza maisha siku 22 zilizopita baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na mafuriko katika eneo la Gandeni mkoani Tanga wakati wakienda kwenye mahafali ya binti huyo.

Lakini uongozi wa shule uliweka mkakati wa kuzuia taarifa hizo zisimfikie hadi amalize mtihani wake wa taifa wa kidato cha nne.

Wingu la simanzi lilitawala nyumbani kwao Goba, jijini Dar es Salaam jana baada ya Anna kuwasili na kupewa taarifa hiyo ya huzuni.

“Hata nikifaulu sitakuwa na furaha. Nani nitamuonyesha matokeo yangu?” Alilia huku akiuliza maswali.

“Mdogo wangu Lulu matokeo yako ya darasa la nne niliyaona ila yangu hatayaona.”

Ilifikia hatua mchungaji wa Kanisa la Moravian, Hance Mwakisoja aliyekuwa anaongoza ibada nyumbani, kukatisha mahubiri na kuwataka waombolezaji kila mmoja asali, ili kumuombea mtoto huyo.

Wakati wote Anna alikuwa akipungia mkono picha za familia yake zilizokuwa zimewekwa mezani.

“Uliona wapi mtoto mdogo kama mimi anabebeshwa majeneza matano? Nilijua nikitoka shuleni nakuja kumlea mdogo wangu (Grace aliyekuwa na mwaka mmoja) kumbe ameniacha, oooh naumia mimi,” alisema huku akilia.

“Wadogo zangu niombeeni nami nije huko, maisha yaliyobaki nitaishi kwa tabu sana.”

Uongozi wa shule ulimudu kuzuia taarifa za vifo hivyo kumfikia Anna kutokana na kuzuia watu kutoka nje kuingia kuongea na wanafunzi, kuzima internet katika eneo la maktaba ambako wanafunzi huenda kujisomea na kutoruhusu kuangalia televisheni kama ilivyo kawaida yao.

Mmoja wa wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo, Fredrick Doya alisema wazazi walizuiwa kukutana na wanafunzi kwa kuhofia wangeweza kuwa na taarifa na hivyo kuzisambaza kirahisi kwa watoto wengine.

Alisema walimu waliwaambia wanafunzi kuwa wamechukua hatua hizo kwa ajili ya kuwataka wajiandae kwa mitihani ya kumaliza elimu ya sekondari.

Alivyopewa taarifa

Tangu kutokea msiba, Anna alikuwa hajaambiwa chochote.

Lakini alidokeza katika maombolezo yake kuwa alihisi kuna jambo baya limetokea, hasa siku ambayo wazazi wake hawakutokea kwenye mahafali.

“Usiku ule niliamka nikaanza kulia mbona sijawaona? Kumbe mlikuwa mmeniacha. Nilihisi tu kuna kitu si kawaida, baba na mama msije?” alisema.

Juzi Jumamosi baada ya kumaliza mitihani ndugu zake walienda kumfuata, lakini pia hawakumpa taarifa hizo.

Baba yake mdogo, Ibrahim Zambi alisema Anna aliuliza walipo wazazi wake, akajibiwa kuwa wanamsubiri nyumbani kwa kuwa kuna sherehe.

Kila mmoja alikuwa anahofia namna gani mtoto huyo atapokea taarifa hiyo ya huzuni kuhusu familia yake.

Jana saa 10:00 alfajiri, Anna aliwasili lakini gari ikasimama kama mita 100 kutoka nyumbani kwao.

“Alipofika, ilibidi watu wanne wanaume wawili na wanawake wawili wakampokee na hapo ndipo walipomweleza kuhusu kilichotokea,” alisema Ibrahim.

“Baada ya taarifa alilia sana, alishikiliwa hadi nyumbani akaenda kulala kwenye miguu ya bibi yake anayeitwa Anna Kamwela.”

Mtoto huyo alijilaza huku akilia na baba yake mdogo anasema hakupata usingizi mpaka kulipokucha.

“Kulipokucha tulimuacha apumzike mpaka saa 4:00, tukamuandaa kwa ajili ya ibada lakini tunamshukuru Mungu kwa sababu mtihani mkubwa ilikuwa ni namna gani atapokea hizo taarifa,” alisema.

Ibada yazua kilio

Tofauti na ibada nyingi ambazo waliofiwa huwa wanatulia kusikiliza mahubiri, Anna alishindwa kuvumilia.

Alikuwa akilia huku akipungia mkono picha zilizokuwa mezani jambo lililoamsha simanzi kwa waombolezaji.

Mchungaji Mwakisoja alisema japo mtoto huyo anapitia wakati mgumu, Mungu hatamuacha.

“Mwanagu Anna kipindi hiki unapopitia huzuni kama hii Mungu hawezi kukuacha, atakuwa na wewe hatua kwa hatua jipe moyo,” alisema.

Mchungaji huyo alisema akili na mawazo ya Mungu hayachunguziki na kwamba hata anapopita kwenye huzuni, bado Mungu ndiye njia yake.

Aliwataka waombolezaji kutoacha kumuombea mtoto huyo kwa kuwa anahitaji faraja.

Aweka mataji makaburi

Eneo jingine lililofufua simanzi ni wakati mtoto huyo alipokuwa akiweka mataji katika makaburi ya wazazi na wadogo zake ambao walizikwa takriban wiki tatu zilizopita.

Alikumbatia misalaba ya wazazi wake huku akiwasemesha kama vile wanamsikia.

“Baba yangu nisamehe, kama kusingekuwa na mahafali msingeniacha,” alisema Anna.

“(Mama) Ulituzaa kwa uchungu tuje kukusaidia, lakini ona mama, umeondoka na wadogo zangu, nimebaki peke yangu.”

Mchungaji azungumza

Mchungaji Mwakisoja aliiomba familia hiyo kulishirikisha kanisa kila hatua ya maendeleo ya Anna.

“Tuendelee kumuombea ili Mungu asiruhusu roho ya ukiwa moyoni mwake, (bali) amsaidie,” alisema.

Mjomba wake, Rafael Lyimo alisema kati ya hazina ambazo wazazi wa Anna aliacha, ni ndugu hivyo wanapaswa kumsaidia mtoto huyo kwa kila hali.

“Tuendelee kumuombea na kumsaidia kwa sababu anapitioa wakati mgumu sana,” alisema.

Daktari ambaye ni baba wa mmoja wa wanafunzi waliokuwa wanasoma na Anna, Fredrick Doya alisema zipo hatua ambazo mtu hupitia baada ya kupata taarifa ngumu na za simanzi.

Alisema kipindi cha huzuni mtu hata akipewa maneno ya faraja huwa hayafanyi kazi mpaka hatua hiyo ipite.

“Hatua ya kwanza ni kukataa ile taarifa; ya pili ni hasira; ya tatu kubishana kwa kuona kama kweli au si kweli na baadaye mtu anakubaliana na hali halisi,” alisema.

Alisema akishakubaliana na hali halisi, anatakiwa kupewa maneno ya Mungu kisha ya wanasaikolojia kwa ajili ya kumuweka sawa.

Chanzo: mwananchi.co.tz