Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilio cha mtoto Said anayetaabika kitandani kwa mwaka mmoja

39504 Pic+kilio Kilio cha mtoto Said anayetaabika kitandani kwa mwaka mmoja

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ndoto za maisha ya mtoto Said Shaaban (10) sasa zinategemea wasamaria akisema maumivu anayopitia baada ya kuugua kwa maji ya moto mwaka mmoja uliopita, hayavumiliki.

Baada ya kuungua kutokana na kukalia maji hayo, mwanafunzi huyo wa Shule ya Msingi Moringe, Dar es Salaam miguu yake ilipooza na hajawahi kupata matibabu sahihi kutokana na hali ngumu ya kiuchumi ya bibi yake, Julieth Simkanga anayemlea.

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwao Mtoni Mtongani, jijini hapa, Simkanga alisema tangu wakati huo mjukuu wake huyo yupo kitandani akiugulia maumivu.

Alisema wakati akiuguza majeraha ya moto, miguu yake ilianza kukosa nguvu, kupooza na kisha kusinyaa kiasi kwamba hivi sasa hawezi kukaa, kusimama wala kutembea kwa sababu ya vidonda.

“Muda wote ni mtu wa kulala ndio maana vidonda pia haviponi, naombeni msaada mjukuu wangu walau atibiwe, kazi yangu ni kuokota makopo ya maji, haiwezi kunisaidia kumtibu mtoto,” alisema: “Kuna wakati hivi vidonda huwa vinatoa harufu kali lakini zaidi ya kumsafisha na dawa ya maji, hakuna tiba nyingine.”

Akisimulia mkasa huo, Said alisema mwaka mmoja uliopita alianguka kwenye maji ya moto baada ya miguu yake kukosa nguvu akiwa Tanga alikokuwa amekwenda likizo.

“Nilipoanguka nyumbani hakukua na mtu wa kunisaidia nilipiga kelele ndio wakaja waliokuwa wanapita njiani,” alisema.

Alisema bibi yake alimfuata na kumrejesha Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.

“Nilitibiwa vidonda vikapona lakini vikaanza tena kwa sababu miguu ilikuwa haina nguvu na nikawa nalala muda wote,” alisema.

Simkanga alisema kutokana na hali ya mjukuu wake, majirani walichangishana Sh50,000 kwa ajili ya kumkatia bima ya afya lakini hakufanikiwa kwa sababu mjukuu wake hana cheti za kuzaliwa.

Alisema tangu Desemba mwaka jana anafuatilia cheti hicho na fedha iliyokuwa imewekwa kwa ajili ya bima ya afya imeshapungua kwa sababu ya nauli.

“Miguu yake imekakamaa inaonekana pia ana tatizo la mifupa, naomba msaada ili nimpeleke MOI (Taasisi ya Mifupa) naamini huko atapona,” alisema.

Aliiomba Serikali kuokoa uhai wa mjukuu wake ambaye anaamini ikiwa atapata matibabu anaweza kupona na kuendelea na masomo yake kama kawaida.

Jirani wa familia hiyo, Mariam Ramadhani aliyekuwa amemletea bibi huyo Sh2,000 kwa ajili ya chakula cha Said alisema ikiwa mtoto huyo atapata matibabu stahiki anaweza kupona na kurejea shule.

Alisema mtoto huyo amekata tamaa na mara kadhaa amewaomba watoto wenzake wanaoenda kumtembelea kumnunulia sumu akiona kwamba hana thamani ya kuendelea kuishi.

“Kuna siku alikuja mtu Said akaomba hela na kupewa Sh200, mwanagu alipokuja kumtembelea akamwambia, bora afe kuliko mateso anayopata na bibi yake hana uwezo, hata chakula anahangaika,” alisema Ramadhani.

Alisema mwanaye alipokea fedha hizo na moja kwa moja akaenda kumwambia (Mariam) kuwa ametumwa sumu ya panya.

“Mwanangu aliponiambia nilikuja kwa Said nikamsihi asikate tamaa, ipo siku atatibiwa na kupona lakini aliniambia ‘mbona mama yangu amekufa, sipendi kumuona bibi anahangaika’ niliumia,” alisema.

Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Moringa, Evarist Deogratias aliyekuwa anasoma na Said alisema kila siku anaporudi shuleni huwa anapita kumsalimia Said kwa sababu anajua, ipo siku atapona na watenda wote shuleni.

Alisema Said ni rafiki yake tangu walipokuwa darasa la kwanza lakini mwenzake aliugua na kuacha kwenda shule.

Mama wa mwanafunzi aliyeanguka kwenye mti wakati alipotuma kuchuma fimbo mkoani Mbeya, Ramadhani Sesemi alisema kuna watu walimfuata kumueleza habari za Said baada ya kuona mwanaye anaendelea kusaidiwa.

“Ilibidi nije haraka nikaona Said yupo kwenye hali mbaya na anahitaji matibabu, nilimsafisha vidonda vilikuwa vinatoa harufu kali nikaanza kuwapigia watu walionisaidia likiwamo Gazeti la Mwananchi,” alisema Sesemi.

Alisema kwa sababu mwanaye, Amos Gabriel, alipewa baiskeli nyingi za miguu mitatu baada ya watu kuanza kumsaidia, ameamua kumpatia Saidi moja ili badala ya kulala muda mrefu, wawe wanamkalisha.



Chanzo: mwananchi.co.tz