Kisarawe. Tangu walipotenganishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) siku 98 zilizopita, maisha ya watoto pacha, Gracious (Nyamiri) na Precious (Telya) Mkono ni magumu na hayaridhishi.
Mwandishi wa Mwananchi aliyewatembelea watoto hao Jumamosi iliyopita katika Kitongoji cha Kigogo, Kijiji cha Kimara Misale, Wilaya ya Kisarawe, umbali wa kilomita 35 kutoka Ruvu– Vigwaza Barabara ya Morogoro, aliwakuta wakiwa katika nyumba ambayo haina madirisha, zaidi ya mlango huku wakiwa hawana kitanda wala godoro.
Mara baada ya kutenganishwa Novemba 7 mwaka jana, United Bank for Africa (UBA) ilimkabidhi mama wa watoto hao Esther Simon (21) hundi ya Sh16.08 milioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ili kuwawezesha watoto hao kuishi katika makazi bora.
Alipoulizwa kuhusu kutotimizwa kwa ahadi hiyo, meneja masoko wa UBA Tanzania, Brendansia Kileo amesema kuchelewa kujengwa kwa nyumba hiyo kumetokana na kutokabidhiwa rasmi eneo la ujenzi wa nyumba na familia ya pacha hao.
Mbali na hundi hiyo, (UBA) pia iliahidi kuhakikisha watoto hao wanapatiwa bima ya afya ya miaka 10 pamoja na kuwafungulia akaunti yenye akiba ya Sh2 milioni. Kileo amesema tayari wameweka kiasi cha Sh2 milioni katika akaunti ya watoto hao, lakini suala la bima halijafanyika.
Watoto hao wanaoishi katika boma la marehemu babu yao, Mejoli Mkono walifanyiwa upasuaji wa kuwatenganisha katika hospitali hiyo ya Taifa Septemba 23 mwaka jana, lakini maisha wanayoishi sasa huenda yakawa kikwazo kwa ukuaji wao.
“Tangu tumerudi tunalalia ngozi, ni maisha yetu tumeshazoea ila kwa hawa watoto naona ni mtihani kwao kulingana na historia yao,” alisema Esther alipoulizwa kuhusu maisha ya pacha hao.
Licha ya changamoto ya eneo wanaloishi, Esther alisema anakosa mahitaji muhimu kama vile sabuni, pampers (nepi), unga wa lishe na mengine madogomadogo.
“Inabidi muda mwingi niwaangalie, sina shughuli ninayofanya kwa sasa kwa ajili yao, hivyo nateseka kwa kweli sina hata sabuni, nguo za watoto zinakaa wiki mpaka nipate kipande cha sabuni,” alisema. Bibi wa watoto hao (mkwe wa Esther), Aksa Mbega alisema tatizo linalowakabili wajukuu wake ni homa za mara kwa mara, “wakiugua tunawapeleka zahanati iliyopo Kimara Masale wanatibiwa, lakini bado hawajapatiwa bima za afya.”
Alipoulizwa kuhusu ahadi ya nyumba na bima ya afya, mama wa pacha hao alisema hajapatiwa chochote tangu alipofikishwa nyumbani hapo na Hospitali ya Muhimbili.
“Muhimbili walinipatia matibabu mimi na watoto wangu, tulikaa huko kwa kipindi chote wakiniahidi kuwa pindi atakapotokea msamaria mwema wa kunisaidia nitarudi nyumbani, kweli walikuja na kutoa msaada nikaletwa mpaka hapa, sasa tangu hapo sijapokea kitu,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu kutotimizwa kwa ahadi hiyo, meneja masoko wa UBA Tanzania, Brendansia Kileo alisema kuchelewa kujengwa kwa nyumba hiyo kumetokana na kutokabidhiwa rasmi eneo.
“UBA imetenga kiasi cha Sh15 milioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba. Tumekuwa tukisafiri kwenda Kisarawe kuwaona na kupata mrejesho sahihi wa eneo, lakini bado maamuzi ya mwisho hayajaafikiwa na familia. UBA ipo tayari kuanza ujenzi pindi tu maamuzi yatakapotolewa kuhusu sehemu ya ujenzi,” alisema Kileo.
Mwananchi ilipohitaji kufahamu kuhusu hali duni kimaisha ya pacha hao na kwanini hawajatoa msaada kujikwamua alisema, “ahadi ya Sh2 milioni imetimizwa na akaunti ya akiba ya watoto U–Care ilifunguliwa rasmi kwa majina ya watoto na ikawekwa pesa taslimu Sh2, 010,112 . Hadi Februari 11, 2019 ipo haijaguswa, fedha iliyochangwa na wafanyakazi wa UBA kwa ajili ya akiba na matumizi ya mapacha na familia kulingana na mahitaji. Mama wa mapacha anajua kuhusu akaunti hii na pesa zilizoko na ana uwezo wa kuipata na kutumia wakati wowote kulingana na mahitaji.”
Alipoulizwa kuhusu bima za watoto hao alisema, “ahadi ya bima ya afya – UBA inashirikiana na mashirika mbalimbali ya bima ili kupata itakayotimiza mahitaji ya matibabu kwa mapacha na mpaka sasa hatujapata mrejesho rasmi kutoka kwenye mashirika kama kulingana na mfuko wanaostahili watoto kama tulivyotarajia.”
“Tupo na mawasiliano na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo na ili waweze kufikiwa na hata ujenzi ni wapi hasa tujenge lazima tushirikiane na Serikali, fundi ameshapatikana na mwenyekiti wa kijiji tuliwasiliana naye pia.”
Mwegelo hakupatikana kuzungumzia suala hilo kwani kwa siku tatu mfululizo simu yake ama haikupokewa au alijibu akitaka atumiwa ujumbe wa maandishi na kila alipotumiwa ujumbe huo hakujibu.