Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilindi wajipanga kunufaika na misitu

12bbebfa4609451f0b1c5dcf4385ebba Kilindi wajipanga kunufaika na misitu

Fri, 19 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI wilayani Kilindi, mkoa wa Tanga imesema itasimamia ipasavyo fedha zitokanazo na uvunaji wa miti ili ziweze kutekeleza miradi ya maendeleo kusaidia jamii.

Hayo yalisemwa na Katibu Tawala Wilaya ya Kilindi, Warda Maulid wakati alipomwakilisha mkuu wa wilaya hiyo, Sauda Mtondoo kwenye ziara ya kutembelea Msitu wa Hifadhi wa Mbwego uliopo katika kijiji cha Mnkonde.

Alisema serikali imeshatoa agizo la kuanza kwa shughuli za uvunaji katika msitu huo, hivyo ni wajibu wake kusimamia kuhakikisha wananchi wanaona manufaa ya uhifadhi huo kwa fedha zitazopatikana kutekeleza miradi ya maendeleo.

"Hakikisheni fedha mtakazopata zinakwenda kutekeleza miradi kama ujenzi ya zahanati, shule na huduma za jamii na ikiwa tutabaini ubadhirifu serikali ya wilaya hatutaacha mtu wahusika tutawachukukia hatua kali," alisema.

Naye Mkurungenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Gracian Makota alisema licha ya wilaya hiyo kuwa na maeneo makubwa ya misitu, lakini hainufaikia na rasilimali zilizopo kutokana na uharibifu unaofanywa wa ukataji miti hovyo pamoja na shughuli za kilimo na ufugaji.

Hata hivyo, alisema uwapo wa mradi wa kuongeza thamani mnyororo wa mazao ya misitu (FORVAC) wilayani humo umesaidia kuimarisha uhifadhi endelevu.

"Tumekuwa na misitu muda mrefu lakini imekuwa ikiharibiwa tu hivyo tunashukuru kupitia mradi wa FORVAC sasa wananchi wanaona thamani ya uhifadhi kwa ajili ya maendeleo yao endelevu," alisema Makota.

Ofisa Misitu Mkoa wa Tanga, Timotheo Sosiya alisema mradi huo ungeweza kutekelezwa hadi katika vijijji 20 wilayani humo lakini kutokana na kukosa sifa za misitu bora ni vijiji vitano pekee ndio vimeingizwa kwenye mradi.

"Hii inatupa picha kwamba bado tuna wajibu mkubwa wa kulinda, kutunza na kuhifadhi rasilimali zilizoko katika misitu kwa maendeleo endelevu lakini na kujilinda na mabadiliko ya tabia nchi,” alisema.

Mratibu wa Mradi wa FORVAC, Petro Masolwa alisema tathmini waliyoifanya kijiji hicho kinatarajia kupata Sh milioni 290 kila mwaka kutokana na uvunaji wa miti pekee.

Chanzo: habarileo.co.tz