Linaweza lisiwe eneo maarufu kwa kilimo cha mpunga kama yalivyo maeneo ya Ifakara, Dakawa, Mbarali, Kilombero, Kyela, Kahama na mengineyo kadhaa yanayojulikana kwa shughuli nyingi za uzalishaji wa zao hilo.
Wengi wanaijua Wilaya ya Kisarawe kwa umaarufu wa kilimo cha mikorosho, mihogo, nazi na pengine matunda.
Wasichokijua ni kuwa wilaya hiyo iliyopo mkoani Pwani ina maeneo mengi yanayofaa kwa kilimo cha mpunga kikiwamo kile cha kutegemea mvua.
Ukweli huu unadhihirishwa na Hamadi Mumbi, ambaye kwa miaka 10 sasa amekuwa akijihusisha na kilimo hicho hadi kufikia hatua ya kuwa mfano kwa wengine katika kijiji cha Mihugwe.
Anasema alihamasika zaidi kulima mpunga baada ya kujionea faida ya zao hilo alipokuwa akisafiri mikoani.
“Ndipo nilipojua kumbe kilimo kinaweza kukutoa sehemu moja ya maisha kwenda nyingine na ukaendesha maisha yako,” anaeleza.
Pia Soma
- Lima na sindika majani ya mnanaa yanalipa
- Mwakalikamo anavyozisubiri milioni 500 za miche ya michikichi
- Mhitimu wa chuo kikuu aliyejiajiri katika kilimo cha matango
Mumbi angeweza kuamua kulima mpunga baada ya kung’amua fursa ya kilimo hicho katika kijiji chake, lakini anasema hakuwa mchoyo aliwahamasisha wenzake kadhaa kulima ikiwamo kuwapa mbegu takribani wanakijiji 20.
“ Binadamu hatuna budi kutegemeana. Unapokuwa peke yako ni kama kero fulani, lakini mkiwa wengi inarahisisha hata kupata misaada, “ anasema na kuongeza kuwa matarajio yake ni kuwa mkulima wa mfano wa kijiji chake na vijiji vya jirani.
Mpunga unalipa
Kwa mujibu wa Mumbi, kilimo cha mpunga hata kile kinachotegemea mvua kama akifanyacho yeye, kinaweza kumtoa mtu hasa kukiwa na mvua ya kutosha na usimamizi mzuri wa shamba.
“ Mwaka ukiwa mzuri yaani kukiwa na mvua nzuri na pia kukiwa na maandalizi mazuri ya shamba, basi kwa mbegu kama Saro5 ekari moja unaweza kutoa viroba 30 hadi 35. Kwa mbegu zetu za asili kama Kampe unaweza kutoa gunia 25, 20 hadi 15, “ anasema.
Kuhusu soko anasema mkulima anaweza kuuza mpunga ghafi akiwa shambani au akausafirisha na kuukoboa akauza mchele.
Kwa kawaida anasema wakati wa mavuno kiroba kimoja huuzwa kwa sio chini ya Sh100,000.
Upo uuzaji mwingine pia maarufu kwa jina la madebe ambapo mpunga hupimwa katika ndoo ya ujazo wa lita 20 na kuuzwa kwa sio chini ya Sh10,000.
Hata hivyo, soko huwa zuri zaidi ikiwa mkulima atauhifadhi mpunga na kuja kuuza baadaye kwa bei nzuri zaidi.
Ni dhahiri kwa mchanganuo huu wa mavuno na bei ya soko, zao la mpunga linaweza kuwatoa wengi.
Hata hivyo, Mumbi bado analalamika kuwa kijijini kwake pamoja na kuhamasisha sana kupitia mikutano ya kijiji, bado hakujawa na mwamko mkubwa wa wananchi kuwekeza katika kilimo cha mpunga.
Tangu aanze kilimo hicho miaka kumi iliyopita, Mumbi anajivunia mafanikio kadhaa yatokanayo na kilimo cha mpunga.
Anasema kupitia mpunga ameweza kujenga nyumba ya kisasa, kusomesha watoto na pia kukuza shughuli za kilimo kwa kuanzisha ufugaji wa wanyama.
Anasema kwa sasa ana ng’ombe wapatao 20, mbuzi na kondoo 20 achilia mbali mifugo mingine kama kuku.
Mumbi ambaye ameweza kuwavutia wenzake watatu ambao sasa wanalima ekari kumi kila mmoja, anasema wakulima wengi wa mpunga wanakosa mavuno kwa kutozingatia maandalizi ya shamba, kupanda kwa wakati, kufanya palizi na kutotumia mbegu bora za mpunga.
Wito kwa Serikali
Anaiomba Serikali iwatazame kwa karibu wakulima wadogo kwa kuwapatia utaalamu wa masuala ya kilimo.
Unaweza kuwasiliana naye kwa ushauri wa kilimo cha mpunga kupitia namba: 0785138900