Mkoa wa Kilimanjaro umepokea Sh6.1 bilioni katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2021 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya elimu, ikiwamo kujenga madarasa, vituo shikizi pamoja na mabweni lengo likiwa ni kuboresha mazingira ya kusomea na kufundishia ili kukuza taaluma.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Abbas kayanda kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai wakati akiwasilisha taarifa ya mkoa juu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2021 katika mkutano wa kawaida wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Kilimanjaro.
Amesema kati ya fedha hizo Sh5.5 bilioni zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 276 ya shule za sekondari katika halmashauri zote za mkoa ambapo kila darasa limegharimu Sh20 milioni huku 360 milioni, zikitumika kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 18 katika vituo shikizi sita kwenye halmashauri za Mwanga, Rombo, na Siha na sh 240milioni zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa mabweni matatu katika halmashauri za Mwanga, Moshi na Same.
"Utekelezaji wa ujenzi wa madarasa unaendelea vizuri kwani miradi mingi ipo katika hatua ya mwisho za umaliziaji , hivyo napenda kuwahakikishia wajumbe wa kikao hiki kwamba mkoa unaendelea kusimamia na kuhakikisha kwamba miradi yote inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kwa kuzingatia muda uliotolewa na serikali,"amesema DC Kayanda.
Akizungumzia sekta ya afya, amesema serikali imeweka mkazo katika upatikanaji wa dawa muhimu, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vipatavyo 227, vinavyojumuisha vituo vya serikali na vituo binafsi.
"Serikali imeendelea na uboreshaji wa miundombinu ya afya na udhibiti wa magonjwa ya mlipuko hususan ugonjwa wa UVICO-19 ambao tumeupa mkazo mkubwa katika kipindi hiki na katika kufanikisha hayo Serikali imeendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya afya katika kospitali ya rufaa ya mkoa Mawenzi, hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati".
Aidha amesema Serika kupitia mpango maalumu ya kupambana na Uvico-19 fedha zimetolewa kwa ajili ya kujenga na kuimarisha miundombinu ya afya ya msingi, ambapo kupitia mpango huo Sh600 milioni zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya huduma za dharura katika halmashauri za Same na Rombo.
Amesema Sh100 milioni zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya wagonjwa mahututi katika halmashauri ya wilaya ya Mwanga na Sh 360 milioni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya watumishi wa afya.
Aidha amewataka viongozi wote kuanzia ngazi za vijiji, kata, wilaya na Mkoa kwa ujumla wake kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi madhubuti wa matumizi ya rasilimali za nchi, ubora na kasi ya utekeleezaji wa miradi katika sekta za jamii na kiuchumi ili kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi wote.
Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amewataka viongozi wote kumuunga mkono Rais wa Tsnzania Samia Suluhu Hasan katika utekekezaji wa ilani ya uchaguzi na kuwaasa wenyeviti wa Halmashauri na madiwani mkoani humo, kubeba agenda za wananchi na kuepuka kubeba agenda binafsi.
"Tumuunge mkono Rais Samia Suluhu kuwatumikia wananchi ambao mwaka 2020 tulizunguka nchi nzima na kuweka nao mkataba wa miaka mitano, kazi ile tuliyopewa tunatakiwa tuwape majibu, ili inapofika mwaka 2025 maswali yapungue na tuende na mpango mpya na wenye ubora zaidi kuliko ambao tunao kwa sasa"amesema Boisafi.