Mkoa wa Kilimanjaro umetengewa Sh15.5 bilioni kwa ajili ya usambazaji huduma ya maji vijijini, hatua ambayo itatatua changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo, katika baadhi ya vijiji mkoani humo.
Hayo yamebainishwa na Meneja Wakala wa Maji na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) Mkoa wa Kilimanjaro, Weransari Munisi wakati akizungumza kwenye kikao cha robo ya kwanza ya mwaka 2021/2022 kilichofanyika wilayani Mwanga.
Munisi amesema katika fedha hizo Sh3.5 bilioni, zinatokana na fedha zilizotolewa kwa ajili ya kupambana na Uviko-19, huku Sh 12 bilioni zikiwa ni fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022
Amesema tayari wameshatangaza zabuni 28 kwa ajili ya utejekezaji na usambazaji wa maji vijijini, na kwamba kukamilika kwa miradi hiyo, kutaongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kwa Mkoa huo.
"Serikali kwa mwaka huu wa fedha 2021/2022, imetenga Sh12 bilioni kwa ajili ya kusambaza maji vijijini na tayari mpaka sasa tumeshatangaza tenda za miradi zipatazo 28 kwa ajili ya kutatua changamoto ya upungufu mkubwa wa maji," amesema.
Ameongeza kuwa "Kupitia mpango wa Serikali wa mapambano ya Uviko, Mkoa wa Kilimanjaro kwa upande wa maji umepatiwa Sh3.5 bilioni zitakazoongezwa kwenye bajeti ya Sh12 bilioni na kufanya Kilimanjaro kuwa na Sh 15.5 bilioni na kazi hizi zinakamilika katika mwaka huu wa fedha."
Aidha, amesema mkoa wa Kilimanjaro wenye zaidi ya watu 1.9 milion ina upatikanaji wa maji wa asilimia 83 vijijini na asilimia 91 mijini, ambapo mji wa Moshi ni asilimia 100, Mwanga 62 na Same asilimia 42 na malengo ni kufikia asilimia 85 kwa vijijini na mijini asilimia 95 ifikapo mwaka 2025.
"Kilimanjaro tuna imani ya kufikia malengo ifikapo mwaka 2025, kwani Mwanga na Same ambao ndo wako chini kwa upande wa miji.
“Utekekezaji wa mradi mkubwa wa maji unaotekekezwa na Serikali wa Same-Mwang-Korogwe utakapokamilika, miji yote miwili itakuwa na uhakika wa kupata maji kwa asilimia 100," amesema Munusi
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Abdallah Mwaipaya amesema hali ya upatikanaji wa maji kwa wilaya hiyo, siyo wa kuridhisha, ambapo ameielekeza Ruwsa kuipitia upya miundombinu hasa ya usambazaji wa maji kwa wananchi.
"Niwaelekeze Ruwsa, kabla ya kutekekeza miradi mipya, wakamilishe viporo vya 2020/2021 lakini pia wapitie upya miundombinu yao hasa ya usambazaji wa maji kwa wananchi kwa kuwa imekuwa ni changamoto kubwa, kutokana na uchakavu wa miundombinu," amesema DC Mwaipaya.