Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilichopo nyuma ya pazia ndoa ya vikongwe wa miaka 102, 90

IMG 4364.jpeg Siri ya ndoa ya vikongwe wa miaka 102, 90

Fri, 23 Jun 2023 Chanzo: Mwananchi

“Pamoja na kutengeneza maisha yangu ya kiroho ili nikifa ninakutane na Mungu, uamuzi wa kufunga ndoa katika umri mkubwa pia unalenga kuikutanisha familia pamoja kwa kuwa imetawanyika na haijakaa pamoja kwa kipindi kirefu.’’

Hiyo ni kauli ya Mzee Masasila Kibuta (102), alipozungumzia uamuzi wa yeye na mke wake Chem Mayala (90) kufunga ndoa katika umri mkubwa walionao.

Vikongwe hao, wakazi wa Kijiji cha Nyamazugo Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza wameingia kwenye historia ya wenza wenye umri mkubwa kufunga pingu za maisha katika Kanisa Katoliki Kigango cha Nyamazungo Parokia ya Ngomamtiba wilayani Sengerema.

Ndoa hiyo iliyozua gumzo miongoni mwa waumini na wakazi wa ndani na nje ya Sengerema ilifungwa mbele ya Padri Julian Mondula wa Parokia ya Ngomamtimba, Juni 17, mwaka huu.

Akizungumza na katika mahojiano maalumu nyumbani kwake kuhusu ndoa yao, Kibuta, mwenye watoto 10, anasema kwa kipindi kirefu, familia yake haijakutana pamoja na amekuwa akitafuta fursa ya kuikutanisha kwa kuitisha vikao bila mafanikio.

“Mimi na mke wangu Chem tumejaaliwa kupata watoto 10 na tunao wajukuu 86 na vitukuu 50, lakini kwa kipindi kirefu hatujawahi kukutana uso kwa uso kama familia; jambo ambalo lilikuwa likitunyima amani kwa sababu hata tukiitisha vikao wana familia wote hawafiki,’’ anasema Mzee Kibuta.

Kabla ya kufunga ndoa hiyo, mzee Kibuta alikuwa na mke wa kwanza aliyefariki dunia na kumuachia watoto wawili na baadaye alipompata mke aliyenaye hivi sasa alizaa naye watoto 10.

Kutokana na kuamini sherehe ya ndoa yao ingewavutia wengi, yeye na mke wake walifikia uamuzi wa kubariki ndoa yao ili kukamilisha agano la kiimani na wapate fursa ya kuikutanisha familia.

“Tulipowashirikisha watoto wetu uamuzi wetu wa kufunga ndoa, wengi wao hawakuamini….walidhani ni utani au akili za uzee. Lakini sisi hakika tulidhamiria na tunamshukuru Mungu tumetimiza nia hiyo,’’ alisema Alisema akishirikiana na mke wake Chem, waliamua kumshirikisha wazo hilo mtoto wao anayeitwa Yunis Masasila, huku lile wazo la kukutanisha familia pamoja kupitia sherehe za ndoa hiyo wakilifanya siri yao wawili.

“Hakuna hata mtu mmoja aliyefahamu siri ya kulenga kutumia sherehe ya harusi yetu kama njia ya kukutanisha watoto, wajukuu na vitukuu, hii tuliifanya siri ya mimi na mke wangu tu na hakika Mungu ametujaalia kulifanikisha,’’ alisema Mzee Kibuta kwa kujisifia.

Japo watoto wote hawakuhudhuria hafla ya ndoa ya vikongwe hao, kimahesabu, lengo lao la kukutanisha familia lilifanikiwa baada ya watoto tisa kati ya 12 kuhudhuria, huku watatu walioshindwa kufika wakipata udhuru kutokana na ugonjwa.

Mzee Kibuta anasema wajukuu wake 50 kati 86 walihudhuria sherehe ya ndoa yao ambayo pia ilihudhuriwa na vitukuu 30 kati ya 50.

Huku akimmwagia sifa mkewe Chem, Kibuta anasema licha ya kukutanisha familia, uamuzi wao wa kufunga ndoa umewapa fursa ya kutengeneza maisha yao ya kiroho.

"Tumeishi kwa kipindi kirefu, tumeishi kwa amani, upendo na furaha. Lakini hatukuwahi kufunga ndoa kanisani, licha ya kuwa ni waumini wazuri na waaminifu wa Kanisa Katoliki,’’ alisema

Aliongeza; “Sasa tumefanikiwa kuhalalisha unyumba wetu kwa kufunga ndoa rasmi kanisani. Tunamshukuru Mungu kwa kufanikisha hili."

Mke afunguka

Chem Mayala, amesema siri waliyonayo ni kushirikiana kwa kila jambo na kusikilizana. Amesema hadi kufikia uamuzi wa kufunga ndoa ni mchakato waliouanza kwa muda mrefu uliokuwa unakwamishwa na tatizo la upungufu wa chakula ambao ulisababishwa na kuchelewa kwa mvua kunyesha. “Baada ya watoto wetu kupata mavuno mwaka huu, tuliamua kufunga ndoa ili watimize agano lako ambalo mungu aliliweka” alisema.

Watoto hawakuamini

Mashauri Masasila ni miongoni wa watoto 12 wa Mzee Kibuta ambaye hakuamini iwapo ni kweli wazazi wao walidhamiria kufunga ndoa katika umri wao mkubwa kwa kuamini pengine kauli zao zilitokana na uzee.

“Tofauti na masuala mengine wanayoyazungumza na kuyaachia njiani, hili la kufunga ndoa walilishikilia na kulisisitiza kila mara, walitulazimisha kuanza kufanya mchakato wa kulifanikisha kutimiza furaha yao,’’ anasema Mashauri.

Anasema kutokana na msisitizo wa vikongwe hao, yeye, ndugu zake wa kuzaliwa tumbo moja kwa kushirikiana na ndugu wengine walianza kukusanya fedha za kugharimia harusi ya wazazi wao.

“Tumefanya maandalizi ya sherehe hii kwa takriban miezi mitatu. Tunamshukuru Mungu tumelifanikisha na wazazi wetu wamefurahi,’’ anasema Mashauri.

Sherehe ya ndoa ya wawili hao iligharimu Sh2.2 milioni, huku ng’ombe wawili wakichinjwa kwa ajili ya kitoweo kilicholiwa kwa pamoja na wali uliotokana na kupikwa kwa kilo 150 za mchele.

“Gharama zote zilibebwa na sisi wanafamilia, hatukuchangisha watu wa nje,’’ anasema Mashauri. Mtoto mwingine wa Mzee Kibuta aliyejitambulisha kwa jina la Yunis Masasila, anasema ndoa ya wazazi wao siyo tu imekuwa gumzo ndani na nje ya kijiji chao, bali pia imewaletea heshima katika jamii.

Naye Andrew Girigimba, ambaye ni mmoja wa vitukuu vya Mzee Kibuta na mkewe Chem anasema ndoa ya vikongwe hao imewapa funzo kubwa kuhusu umuhimu wa kukamilisha agano la kiimani kwa kufunga ndoa.

“Maisha yao ya kuishi kwa upendo licha ya umri wao mkubwa ni funzo kwetu siku zote kila tunapowaona; lakini hili la wao kufunga ndoa katika umri wao huu mkubwa ni funzo kubwa zaidi kwetu vijana. Binafsi nitaiga na kufuata nyayo za babu na bibi,’’ anasema Andrew

Padri apigilia msumari

Akitoa mafundisho ya kiimani wakati wa hafla ndoa ya vikongwe hao, Padri Jualian Mundula amewataka vijana ambao wengi wao wanaishi kinyumba bila kufunga ndoa kuiga mfano wa mzee Kibuta na mkewe Chem kwa kutengeneza maisha yao ya kiimani kwa kufunga ndoa.

“Uamuzi wa wazee hawa wa kufunga ndoa katika umri wa miaka 102 na 90 ni wa kupongezwa sana; ni uamuzi wa kijasiri unaofaa kuigwa na kila mwenye mapenzi mema,’’ anasema Padri Mundula

Chanzo: Mwananchi