Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kila mfiwa, walionusurika Mv Nyerere kupata Sh1 milioni kila mmoja

19145 Mfiwa+pic TanzaniaWeb

Tue, 25 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameagiza wafiwa wote waliopoteza ndugu zao kwenye ajali ya kivuko cha Mv Nyerere kupata Sh 1 milioni baada ya awali kupewa Sh 500,000 kila mmoja.

Hata hivyo watu 41 walionusurika kwenye ajali hiyo nao watapewa Sh1 milioni kila mmoja.

Fedha hizo zinatokana na michango ya kampuni, watu na taasisi mbalimbali wanaoendelea kujitokeza kuchangia waathirika hao.

Awali, familia za waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo iliyotokea Alhamisi iliyopita walipewa Sh500,000 kwa kila mtu aliyefariki, fedha ambazo zimepatikana kutokana na michango ya Watanzania, kampuni na taasisi mbalimbali.

Akizungumza na vyombo vya habari jana kisiwani Ukara wilayani Ukerewe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaac Kamwelwe alisema leo wataanza kutoa fedha hizo kama walivyoagizwa na Rais Magufuli kwa familia za marehemu na wote walionusurika.

“Rais ameniagiza niwaambie kwamba fedha kwa waliopoteza ndugu zao na wale 41 walionusurika, sasa watapata Sh1 milioni kila mmoja. Kuanzia kesho (leo) tutaanza kutoa fedha hizo, wapeni taarifa,” alisema Kamwelwe.

Alisema kiwango cha fedha kilichokusanywa mpaka jana jioni ni Sh397 milioni ambazo zimetolewa na watu na taasisi mbalimbali. Alisema Rais Magufuli amesema fedha hizo ni za wananchi walioathirika na ajali hiyo.

Waziri huyo alisema mpaka kufikia jana jioni, miili miwili ya watoto ilipatikana wakati kazi ya kukiinua kivuko hicho ikiendelea na kufanya idadi ya waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo kufikia 226.

Kuhusu kurudisha hali ya usafiri katika kisiwa hicho, Kamwelwe alisema leo au kesho kitapelekwa kivuko kingine kinachoitwa Mv Temesa ambacho kiko Mwanza kwa ajili ya kutoa huduma wakati shughuli ya kukiinua kivuko cha Mv Nyerere ikiendelea.

Naye Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo alisema wana matumaini kivuko cha Mv Nyerere kitatoka salama na kitafanyiwa uchunguzi kisha kiendelee kufanya kazi kama kawaida.

Alisema kazi kubwa inafanyika kuhakikisha hali ya usafiri inakuwa ya kawaida.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisisitiza kuanzia leo, Serikali itaanza kutoa Sh1 milioni kwa wafiwa na walionusirika wote na kuwahimiza wananchi wawafikishie taarifa waliokwenda kuzika sehemu nyingine.

Chanzo: mwananchi.co.tz