Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amewakumbusha vijana nchini kuendelea kuchukua tahadhari na kujikinga dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi (VVU) kwa kutumia kinga.
Hayo ameyasema leo Julai 14, wakati akiwaaga wapanda mlima 36 na waendesha baiskeli 25 ambao wameanza safari ya kuupanda mlima Kilimanjaro kwa siku 7 kupitia geti la Machame kwa lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi kupitia kampeni yake ya 'GGM Kili change 2023'.
"Bahati mbaya maambukizi mapya yanatokea kila siku na hasa kwa vijana, na kwamba katika maisha ya mwanadamu ni lazima mtu apitie hatua hiyo lakini ndugu zangu asali ile ina sumu, ni lazima kuchukua tahadhari," amesema Kikwete na kuongeza;
"Nilipokuwa Rais kila mara nilikuwa naendesha sana kampeni kukumbusha Watanzania wenzangu kwamba Ukimwi ni maradhi ya kujitakia, si maradhi ya bahati mbaya, tusimsingizie Mwenyezi Mungu hapana, kwasababu ukiacha mtu labda aliyepata bahati mbaya ya kuongezewa damu isiyo salama, lakini njia kuu inayosambaza Ukimwi tunapanga mahali pakukutana, siku na saa ya kukutana labda aliyebakwa tu."
Kwa mujibu wa Rais huyo mstaafu, ikiwa watu wamepanga panga kukutana, basi ni vema kukumbusha kutumia kinga.
“…unamwambia mwenzako utaleta wewe au nileta mimi na akikwambia ataleta…chukua yako tia mfukoni kama mwanaume, kama mwanamke weka yako kwenye pochi ukirudi uko salama salimini, lazima tuendelee kukumbushana na vijana ni lazima muendelee kukumbushana kwamba ukimwi bado upo," amesema.
Aidha amesema lengo la Serikali kupitia kampeni ya 'GGM Kili challenge' ni kuhakikisha ifikapo 2030, kunakuwepo na zero 3, ambazo ni katika kupunguza maambukizi mapya ya Ukimwi, unyanyapaa na kubagua watu wanaoishi na VVU na kupunguza vifo vitokanavyo na Ukimwi.
Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong ameishukuru Serikali kwa kuwaunga mkono katika kampeni hiyo ya kupambana na maambukizi mapya ya virusi hapa nchini na kwamba lengo lao ni kuona tatizo linamalizika.