Rais mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete jana Julai 15, 2023 alizitembelea familia za marehemu Basil Mramba, Michael Shirima na Isdori Shirima, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro huku akisisitiza waliobaki katika familia hizo wanayaenzi na kuendeleza waliyofanya wazee wao katika Taifa.
Michael Shirima, alikuwa Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya shirika la ndege la Precision Air alifariki dunia, Juni 9 mwaka huu katika hospitali ya Aghakan Dar es salaam, Basil Mramba aliyewahi kuwa Mbunge wa Rombo na Waziri wa Fedha alifariki Agosti 17, 2021 kwa ugonjwa wa Uviko 19 na Isdori Shirima ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, aliyefariki Machi 31 mwaka huu.
Kikwete amesema marehemu ni miongoni mwa watu muhimu katika maisha yake kwa kuwa alishirikiana nao katika mambo mengi katika Taifa.
"Katika maisha yangu na hasa katika maisha ya siasa kuna watu ambao nilifanya kazi nao kwa karibu na bahati mbaya sikubahatika kushiriki kwenye mazishi yao wala kutoa heshima za mwisho, hivyo leo nikasema ni fursa nzuri niwahani familia na kuweka mashada ya maua,"amesema
"Nimekuja hapa nyumbani kwa Mramba leo, nitakwenda kwa Isdori Shirima ambaye tulikuwa naye kipindi kile akiwa Mkuu wa Mkoa, lakini mwaka 1995 nilipogombea mara ya kwanza Isdori Shirima ndiye alikuwa wakala wangu kwenye kuhesabu kura kule Chimwaga, ni wenzangu sana, ni watu ambao nilikuwa nao karibu,”amesema.
“Mramba nimekuwa naye kwa muda mrefu na Michael Shirima nimekuwa naye karibu sana, lakini ameandika kitabu cha maisha yake 'On my father's wings' na mimi nimeandika dibaji ya kile kitabu chake,"ameongeza.
Aliongeza"Watu hawa ambao nimekuja kuwatembelea leo ni watu ambao nimekuwa nao karibu sana maishani , sikubahatika kuja kutoa salama za heshima kwao na kwenye mazishi yao, hivyo nimepita kutoa pole kwenye familia, kupita kwenye makaburi yao niwaombee,"
Akimshukuru Rais Kikwete, Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuja kwake Rombo kuhani kwenye familia hizo ameonyesha upendo mkubwa na kuthamini wale waliotoa mchango kwa Taifa.
"Tunajivunia sana maisha ya viongozi wetu hawa kwa alama walizoziacha katika Taifa hili, Mheshimiwa Rais (mstaafu) kwa kuja hapa leo umeonyesha upendo mkubwa sana kwa Warombo, tunakushukuru sana,"amesema Profesa Mkenda
Godfrey Mramba, ambaye ni mtoto wa aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba amemshukuru Kikwete na kusema familia imefarijika sana kwa kutambua mchango wa baba yao.
"Tumefarijika sana kuona uko pamoja na sisi kwa kumuenzi baba yetu, tunakushukuru mno, tunakuombea kila la kheri,"amesema