Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kikongwe wa miaka 80 auawa, nyumba yake yateketezwa moto

Bibi Auawa Aef Kikongwe wa miaka 80 auawa, nyumba yake yateketezwa moto Manyara

Mon, 30 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkazi wa Kijiji cha Changombe, wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara, Nelson Lotisia Mollel (80), ameuawa kisha nyumba yake kuteketezwa kwa moto na watu wasiojulikana.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumapili, Oktoba 29, 2023 ikiwa ni siku chache zimepita tangu kikongwe huyo aliposhinda kesi ya mgogoro wa ardhi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, ACP George Katabazi amethibitisha tukio hili akisema lilitokea usiku wa kuamkia leo wakati mzee huyo akiwa amelala ndani peke yake.

"Mzee alivamiwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo, walichoma nyumba yake na alipotoka nje alishambuliwa na vitu vyenye ncha kali vilivyosababisha kutokwa damu nyingi kisha kufariki dunia," amesema ACP Katabazi

Amesema baada ya watu hao kutekeleza tukio hilo walitoweka huku wakiwa wamehakikisha vitu vyote vilivyokuwa ndani ya nyumba vimeteketea kwa moto.

"Hakuna hata kitu kimoja kilichobaki ambacho watu wameokoa na wakati huo marehemu alikutwa nje akiwa amelala akitokwa damu nyingi baada ya kupata jeraha kubwa kichwani na mgongoni ambayo yamemsababishia kifo," amesema ACP Katabazi

Kamanda huyo amesema marehemu alikuwa anadai watu wengi fedha aliwakopesha na pia alikuwa na kesi ya mgogoro wa ardhi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ambayo imemalizika siku mbili kabla ya kifo chake.

Amesema alipata ushindi na alipofika nyumbani kwake alishinda siku moja kisha kukutwa na umauti.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Changombe, Mohaned Issa akizungumzia tukio hilo amesema alipata taarifa saa sita usiku akiwa amelala kuwa nyumba inaungua na alipofika alikuta watu wakizima moto huku mzee huyo akiwa anabubujikwa na damu nyungi.

"Mzee huyu alikuwa amelala pembeni huku damu nyingi zikiwa zinamtoka kichwani na mgongoni na baada ya muda mfupi alipoteza maisha na wakati huo nyumba yake ilikuwa inawaka moto," amesema Issa

Kamanda Katabazi ametoa wito kwa jamii kuacha tabia za kujichukukia sheria mkononi akisema hata kama mtu ana kosa ni vyema kuacha sheria ifuate mkondo wake.

"Mpaka sasa tunamshikilia mtu mmoja kwa upelelezi na huyu atatusaidia undani wa tukio hili na tabia za watu kujichukulia sheria mkononi zimeendelea kujitokeza, Jeshi la Polisi tutahakikisha wale wote waliohusika tunawakamata," amesema ACP Katabazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: