Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kikongwe apokea Sh78 milioni, kuwekeza kwenye kilimo, kujenga nyumba

81727 Pic+kikongwe Kikongwe apokea Sh78 milioni, kuwekeza kwenye kilimo, kujenga nyumba

Fri, 25 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Licha ya kuwa na miaka 98, Bibi Nasi Muruo mkazi wa Sinoni, jijini Arusha aliyenyang’anywa ardhi yake tangu mwaka 1977 na kurejeshewa Agosti mwaka huu, amepanga kuwekeza katika kilimo na kujenga nyumba mpya.

Kikongwe huyo ambaye hadi jana alikuwa amepokea Sh78 milioni kutoka kwa kaya tisa kati ya kaya 110 zinazotakiwa kumlipa Sh519.3 milioni baada ya kuvamia eneo lake la ekari nane, alisema anakusudia kujenga nyumba mpya, kufungua duka la bidhaa za nyumbani, kununua mashamba na trekta kwa ajili ya kulimia.

“Nikipata fedha hizi kwa kuwa nimepata shida sana kukaa chumba kimoja cha kupanga miaka 42 kwanza nitajenga nyumba na kufungua duka, lakini nitahitaji chakula cha wajukuu zangu hivyo nitanunua matreka na mashamba ili nilime,” alisema.

Akizungumza na Mwananchi jana, bibi huyo alisema anashukuru kaya zilizoanza kumlipa na ana imani ifikapo mwisho mwa mwezi Novemba kaya nyingi zitakuwa zimemlipa.

“Nawashukuru sana Rais (John) Magufuli na Waziri (William) Lukuvi, nimeanza kupata haki yangu baada ya kuitafuta kwa miaka 42 na nikipata fedha hizi nakusudia kujenga nyumba, kufungua duka na kununua treka na kuanzisha mashamba ili nilime na wajuu wangu,” alisema.

Tayari wajukuu wa bibi huyo, wanaendelea na ujenzi wa nyumba ya kuishi kwa muda bibi huyo, nyumbani kwao wilayani Monduli, ili ahame katika nyumba aliyopanga chumba kimoja.

Pia Soma

Advertisement
Obedi Saiteru mmoja wa wajukuu hao, alisema wana imani hivi karibuni watakamilisha nyumba ya bibi huyo, kukaa wakati akiendelea kusuburi fedha zake zote na kuondokana na maisha ya kupanga.

Agosti 28 mwaka huu, Waziri Lukuvi alizipa miezi mitatu inayomalizika Novemba mwaka huu, kaya 110 zilizojenga kwenye ardhi ya bibi huyo kumlipa Sh519.3 milioni, kulingana na ukubwa wa kila kaya la sivyo nyumba zao zitabmolewa na bibi huyo kukabidhiwa ardhi yake.

Katibu Mkuu wa Kanisa la Evengalistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Askofu Dk Leonard Mwizarubi alikuwa wa kwanza, kulipa kiasi cha Sh69 milioni kwa bibi huyo kutokana na kuwa eneo la eneo la mita za mraba 3,458.

Askofu Mwizarubi alisema kanisa limelipa fedha hizo, kutekeleza maagizo ya serikali kwa kuamini kuwa bibi huyo, alikuwa na haki zote za umiliki wa eneo hilo ambalo alikuwa akigombania na ndugu yake.

“Kama kanisa tunampongeza Rais John Magufuli kwa uamuzi wa kumpa haki bibi huyu na sisi tunamuunga mkono,” alisema.

Alisema kwamba kanisa hilo, limejiondoa kuitwa wavamizi katika eneo hilo na sasa ni wakazi halali na anatarajia watapewa hati ya umiliki wa ardhi hiyo.

Maagizo ya Serikali

Waziri Lukuvi alisema ndani ya miezi mitatu, kila kaya itatakiwa kulipa fedha hizo, kulingana na eneo lake, ambako kila mita moja ya mraba watapaswa kulipia Sh 20,000 na eneo lenye makazi lina jumla ya ekari 6.4 ambazo zimejengwa na eneo la wazi lililobaki bila kujengwa amekabidhiwa bibi huyo.

Waziri Lukuvi, alisema Serikali imechukua uamuzi huo, kwa kutambua familia nyingi zilizouziwa eneo hilo ni masikini, kwani ingeweza kuamua kutekeleza hukumu ya mahakama kwa kuwabomolea wote ambao wamevamia eneo hilo.

“Hizi ni huruma za Rais wenu John Magufuli, baada ya kupokea malalamiko ya Bibi Muruo alinituma kuja hapa kumaliza mgogoro huu na sitarudi tena mara baada ya maamuzi haya,” alisema.

Muruo, kwa miaka 42 amekuwa akihangaika kudai, haki yake na licha ya kushinda kesi na kutakiwa kurejeshewa ardhi yake tangu Mei 22, 1979 katika baraza la usuluhishi la ardhi jijini Dar es Salaam na baadaye Mahakama Kuu, kashinda tena kesi dhidi ya ndugu wa familia yake, Edward Lenjashi aliyekuwa amenyang’anywa eneo hilo ambaye alifariki mwaka jana.

Bibi huyo, katika kesi yake alikuwa akitetewa bure na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na gazeti hili Julai mwaka huu, liliripoti habari zake kwa mara ya kwanza ambako aliomba msaada kwa Rais Magufuli na baada ya siku moja tu Serikali iliingilia kati mgogoro huo.

Julai 8, Waziri Lukuvi alifika Arusha, kumsikiliza kikongwe huyo na pande zote baada ya kupata maelekezo ya Rais Magufuli na ndipo Agosti 28 akatoa maelekezo akitaka kaya zote zilizovamia eneo hilo kumlipa fidia kikongwe huyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz