Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kijiji ambacho ni marufuku kunywa pombe

Kijiji Pic Kijiji ambacho ni marufuku kunywa pombe

Fri, 23 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Wakati dunia ikishangazwa na hatua ya Taifa la Qatar kuzuia uuzwaji wa pombe maeneo ya karibu na vilipokuwa viwanja vilivyotumika kuchezewa michuano ya kombe la dunia, sharti kama hilo lipo katika moja ya kijiji hapa nchini.

Katika michuano hiyo, taifa hilo lilizuia uuzwaji wa vinywaji hivyo kwenye maeneo hayo, kwa kile lilichokieleza kuwa si utamaduni wake na hivyo yeyote aliyehitaji alipaswa kwenda mbali kupata starehe hiyo.

Kumbe Qatar ni kama imerudia kile kinachofanyika katika Kijiji cha Songomnara wilayani Kilwa nchini, ambacho kilianza kuweka sharti hilo tangu karne ya 10 (takriban miaka 700 iliyopita).

Hayo yamebainishwa Desemba 22, 2022 na Muangalizi wa Magofu ya hifadhi ya malikale ya Songomnara mkoani Lindi, wakati wa ziara ya Waandishi wa habari katika vituo vya utalii Kusini iliyoratibiwa na Bodi ya Utalii (TTB) kupitia mradi wa REGROW.

"Huu umekuwa utamaduni wa kijiji hiki na ulianzishwa na wazee wetu tangu karne ya 10, katika eneo hili haruhusiwi yeyote kuuza pombe," amesema.

Amefafanua yeyote atakayebainika kufanya biashara hiyo, anaondolewa kijijini hapo kwenda kwingineko kwa kuwa amevunja miiko.

Kulingana na Said, sharti hilo halitokani na miiko tu, bali utamaduni uliowekwa tangu enzi za wazee na hivyo unaendelea kufuatwa hadi sasa.

Si kwamba hakuwahi kutokea aliyejaribu kufanya biashara hiyo, amesema wapo wengi na wote walichukuliwa hatua ya kufukuzwa kijijini wahamie kwingineko.

Kutokana na sharti hilo, ameeleza ni nadra kumuona mlevi kijijini hapo, aghalabu wanaofanya hivyo hujituliza makwao ili wasibainike.

"Sio kwamba watu hawaruhusiwi kunywa pombe hapana. Lakini hapa kijijini haiuzwi hivyo ukitaka kunywa unasafiri kwa boti safari ya masaa mawili hadi zinapouzwa nje ya kijiji," amesema.

Hata hivyo, amesema baada ya kunywa na kulewa unapaswa kurudi kwako kimyakimya bila vurugu.

"Wewe mwenyewe mlevi utaona aibu, huwezi kulewa ukapiga kelele kwa kuwa huku hakuna walevi kwa hiyo atakayelewa atakuja kimyakimya," amesema.

Kuhusu watalii wanaotembelea eneo hilo, amesema wengi huja na vinywaji vyao na hulewa kwa starehe zao, sio kusumbua wengine.

Hata hivyo, amesema utamaduni huo na nyingine kijijini hapo kumekuwa kivutio cha wengi wanaotembelea kwa kuwa si mara zote nchini kuwepo masharti hayo.

Rehema Saidi ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, amesema takriban watu 480 wanaishi kijijini hapo na wapo baadhi ya waliohamishwa kwa kufanya shughuli hizo.

Ameeleza utaratibu huo ameukuta katika Kijiji hicho, hivyo kila anayekuja hana budi kuendana nao.

Lakini, amebainisha tija ya utamaduni huo, akisema vitendo vyote vinavyotokana na ulevi havipo ukiwemo vya wizi na ugomvi.

"Mimi nimeingia hapa Machi mwaka huu, sikuwahi kuletewa ripoti ya wizi au ugomvi kwa sababu hakuna tabia za ulevi, hii imesaidia kuimarisha amani na utulivu kijijini," amesema.

Chanzo: Mwananchi