Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kijana ataka kukutana na Magufuli kumueleza madini yanavyotoroshwa Mirerani

41655 Pic+madiniKijana ataka kukutana na Magufuli kumueleza madini yanavyotoroshwa Mirerani

Thu, 14 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Emmanuel Ibrahim, anayejishughulisha na uchimbaji madini katika mgodi wa Mirerani ameeleza nia yake ya kutaka kuonana na Rais John Magufuli kumueleza jinsi wafanyabiashara na watendaji wa Serikali wanavyoshirikiana kutorosha madini ya Tanzanite.

Amesema licha ya eneo hilo la mgodi kujengwa ukuta, madini hayo yanatoroshwa kupita mlango mkuu, walinzi wa eneo hilo ni miongoni mwa watendaji wa Serikali wanaohujumu jitihada za Rais kuhakikisha nchi inanufaika na madini.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Februari 13, 2019 kijana huyo amesema amefanya jitihada mbalimbali kuhakikisha anafikisha ujumbe huo kwa Rais Magufuli na kuwataja wafanyabiashara wanaotorosha madini hayo.

“Nimetoka Mirerani Januari na kuja Dar es Salaam kwa lengo la kuonana na Rais. Sitaondoka hapa mpaka nikamilishe suala hilo. Januari 3, 2019  nilikwenda Ikulu lakini nikaambiwa siwezi kumwona, niache barua na namba zangu za simu lakini mpaka sasa kimya,” amesema.

Ibrahim anayefanya kzi katika katika kampuni ya Vaneria, amesema hana imani na viongozi wengine wa Serikali kwa sababu alishafikisha suala hilo lakini hawajalifanyia kazi na utoroshaji huo unaendelea.

Amesema alifikisha suala hilo kwa mkuu wa walinzi wa lango kuu ya kuingia mgodini lakini hakutaka kufuatilia na kusema hakuna madini yanatoroshwa.

Baada ya majibu hayo, aliamua kumpigia Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti ambaye naye aliahidi kulifuatilia lakini anaona bado halijatatuliwa.

Amesisitiza kwamba utoroshaji wa madini hayo ni mtandao mpana ambao unahusisha watu wenye nguvu ya fedha na mamlaka serikalini.

Kijana huyo amesema amejitoa mhanga kuhakikisha kwamba anaonana na Rais Magufuli ili achukue hatua kama ambavyo amekuwa akifanya.

 “Nimekuja hapa tangu Januari, sina kazi, ninaishi kwa rafiki yangu tu. Sitaondoka mpaka nimeonana na Rais Magufuli. Hili suala ni kubwa, Rais wetu anatakiwa apate taarifa sahihi kutoka kwetu sisi tunaofanya kazi kule (Mirerani),” amesema.

“Ninahatarisha maisha yangu kwa sababu nataka suala hili liishe. Siku ile Rais Magufuli alipokutana na wafanyabiashara wa madini walimdanganya kwamba wanaotorosha ni wageni, siyo kweli ni Watanzania wenyewe.”



Chanzo: mwananchi.co.tz