Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kijana aliyelelewa kijiji cha mafunzo awa mfano bora katika kilimo

Fdfffe3696f7607a834cbd246394d265.PNG Kijana aliyelelewa kijiji cha mafunzo awa mfano bora katika kilimo

Tue, 15 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAKATI Kijiji cha SOS kilichopo Mombasa, Unguja kikitimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1991 malengo makubwa ya kuanzishwa kwake yanaendelea kuonekana.

Vijiji vya aina hii vipo karibu dunia nzima ikiwamo Tanzania, Austria, Marekani, Afrika Kusini, Pakistan, Canada, Ufaransa, Italia na Ujerumani kwa ajili ya kusaidia watoto. Asili ya jina SOS inasemekana lilianza kama Save Our Ship (Okoa Meli Yetu) lakini wengi wanaamini asili yake ni okoa nyoyo zetu (Save Our Soul).

Vijiji vya SOS vya watoto (Ujerumani huitwa SOS-Kinderdorf) vilianzishwa chini ya shirika lililokuwa huru lisilo na faida. Uendeshaji wake huwezeshwa na jamii, serikali na asasi za kimataifa ili kusaidia kukidhi mahitaji na kulinda maslahi na haki za watoto tangu mwaka 1949 lilipoanzishwa nchini Austria. Kimataifa lilianzishwa mwaka 1960.

Tanzania Bara kijiji hichi kipo karibu na Kituo cha Mabasi (daladala) cha Mawasiliano-Simu 2000 na uendeshaji wake huhusisha nyumba yenye familia ya watoto, mama na baba ambaye ndiye msimamizi wa kituo kizima na kuwapatia watoto malezi kama ya familia na kuwafundisha kujitegemea kwa kuwapa stadi za kazi.

Kijiji hiki cha visiwani Zanzibar, kama vilivyo vingine vya aina hiyo, kilianzishwa ili kuwapatia matunzo na malezi watoto wanaofikishwa hapo kutokana na kupoteza wazazi wao au wengine kukutwa wakiishi katika mazingira magumu yanayowafanya wakose matunzo kulinganisha na wenzao.

Wakiwa kituoni, watoto hawa wanatakiwa pia kupatiwa elimu na huduma za afya, lakini pia kuwapa stadi za maisha ili kuwawezesha kusimama wenyewe katika maisha yao kwa maana ya kujitegemea.

Khamis Ame Baraka ambaye sasa ana umri wa miaka 25 ni miongoni mwa vijana wa kupigiwa mfano waliopitia SOS, yeye akiwa ameishi katika kijiji hicho kwa muda wa miaka 11.

Khamisi, baada ya kujikita katika sekta ya kilimo na ufugaji ni miongoni mwa vijana wa SOS wenye mafanikio na wanaojitegemea.

“Siwezi kukisahau kijiji cha SOS ambacho nakiona sawa na mama yangu mzazi kwa kunilea na kunionesha njia ya maisha ya kujitegemea,” anasema kijana huyo akiwa katika shamba lake la mananasi lililoko Donge Kitaluni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Khamisi amelazimika kuingia katika sekta ya kilimo na ufugaji wa kuku kufuatia mabadiliko ya mageuzi ya vijiji vya SOS duniani kote kuwataka vijana wanaofikisha umri wa mika 18 kuishi nje ya vijiji au katika familia zao za asili.

Anasema alipohitimu darasa la 10 na kushindwa kuendelea na elimu ya sekondari, uongozi wa kijiji cha SOS uliamua kumwendeleza kwa kumpeleka kupata mafunzo ya kazi za kuunganisha umeme majumbani ili baadaye aweze kujitegemea kimaisha na kujiajiri.

Anasema anashukuru kupata mafunzo hayo lakini baadaye aligundua kwamba mapenzi na kiu yake haikuwa huko bali kwenye kilimo na ufugaji.

Anasema kwa nyakati tofauti alipata nafasi ya kuhudhuria mafunzo ya maandalizi ya mashamba ya kilimo cha mbogamboga kuanzia Kizimbani Unguja ambapo alijionea shughuli za kilimo cha matunda mbalimbali na mboga na ‘kumkamata’ sawasawa.

Anasema aliwaomba viongozi wake wa SOS waliompa Sh 100,000 ambazo alizitumia kwa kuanzisha kilimo cha matikiti maji katika eneo la ardhi, ndani ya kijiji cha SOS.

Anasema matikiti hayo yalimwezesha kupata mavuno mazuri yaliyompa matumaini makubwa ya kupata mafanikio katika kilimo.

“Kilimo cha matikiti kilinionesha njia kwamba kumbe naweza kujiajiri katika kilimo na kuweza kuendesha maisha yangu,” anasema kijana huyo.

Anasema mwaka 2019 uongozi wa kijiji cha SOS ulimpatia safari ya mafunzo ili kujua mbinu bora za kilimo cha mboga mkoani Mwanza na aliporudi alikuja na ari mpya ya kuhakikisha sasa anaingia rasmi katika kilimo.

Khamisi anasema Desemba 2019 baada ya kushauriana na viongozi wake wa Kijiji hicho aliandika mpango kazi wa biashara katika kujikita zaidi kwenye sekta ya kilimo. Alikubaliwa na kupewa Sh milioni 2.9 kati ya Sh milioni 4.9 alizoomba.

Anasema alizitumia fedha hizo kwa kujikita kindakindaki kwenye kilimo cha mboga na viungo kama nyanya na bilinganya sambamba na kuanzisha ufugaji wa kuku wa mayai.

Anasema kutokana kilimo cha nyanya pamoja na bilinganya, akafanikiwa kupata Sh milioni sita na hiyo anasema ni kutokana na maandalizi mazuri ya shamba aliyofanya na kutumia mbolea.

“Faida ya wastani wa Sh milioni nne ilininyanyua sana na kunipa moyo na ari kwamba kumbe naweza kuishi maisha mapya ya kujitegemea katika sekta ya kilimo,” anasema Khamisi.

Anasema kuanzia hapo alipanua wigo wa shughuli zake na kujikita katika ufugaji wa kuku wa mayai kwa kuwekeza Sh milioni 1.4 na kufanikiwa kuzalisha zaidi ya Sh milioni 3 baada ya kuuza mayai na kuku wake.

Khamisi anasema kwa ujumla shughuli za kilimo na ufugaji zimemnyookea katika maisha yake na ndiyo chaguo lake kwa sasa huku akitamani vijana wengine kujikita katika sekta hiyo ambayo anasema ni ajira tosha.

Kwa mfano anasema tayari amepata eneo la shamba la mananasi takriban eka mbili na nusu huko Donge Kitaluni, Mkoa wa Kaskazini Unguja ambacho ni kijiji alichozaliwa.

Anasema anatarajia kuvuna matunda hayo kuanzia Oktoba hadi Novemba mwaka huu.

“Shamba moja lenye ukubwa wa eka moja na nusu nimelikodi kwa Sh milioni 1.4 na shamba jingine ni la familia, sasa hapa nikivuna natarajia kuingiza wastani wa Sh milioni 10,” anasema.

Anasema akiondoa gharama za kilimo, ana uhakika wa kuvuka hatua nyingine na kuongeza mtaji zaidi wa kuendelea na kilimo.

Mananasi hustawi vizuri katika maeneo ya Jimbo la Donge, Mkoa wa Kaskazini pamoja na Machuwi, Wilaya ya Kati.

Alipoulizwa changamoto za maisha anazokabiliana nazo hasa baada ya kuondoka katika Kijiji cha SOS na kuanza kujitegemea kimaisha, Khamisi anasema mwanzo alipatwa na hofu kama ataweza kujitegemea kutoka na kuishi kwa miaka 11 ndani ya Kijiji cha SOS huku akiwa haulizwi kitu chochote kuanzia chakula na matumizi mengine.

“Unajua kwa muda wa miaka kumi na moja unaishi kula na kulala wakati mwingine unaulizwa utakula nini nyama au samaki... Sasa unapokwenda kuishi maisha mapya nje ya kijiji mambo hayo hayapatikani tena… Kwa kweli nilihofu lakini sasa sina wasiwasi na maisha hata kidogo,” anasema.

Mkurugenzi wa Kijiji cha SOS, Asha Salim anasema mtoto anayeishi katika vijiji hivyo anatakiwa kuondoka na kuishi nje kwa kutafutiwa makazi akishafikisha umri wa miaka 18.

Anasema anaweza kusaidiwa kukodishiwa nyumba wakati akianza maisha au kurudi kuishi kwa wazazi wa familia yake ya asili.

Asha anasema lengo la programu hiyo ni kuwawezesha watoto ambao walikumbana na changamoto za maisha utotoni kupata malezi na stadi za maisha ili waweze kusimama wenyewe kimaisha.

Anasema SOS inachokifanya ni kuwapatia nyenzo mbalimbali zitakazowawezesha kujitegemea ikiwemo elimu, maadili na stadi za maisha.

Anakiri kwamba Khamisi ni miongoni mwa vijana walioonesha uwezo mkubwa wa ubunifu na kujituma baada kujiingiza katika kilimo cha mazao ya biashara kiasi cha sasa kuweza kusimama mwenyewe kimaisha.

“Matarajio yetu ni kuona vijana wengi wakifuata nyayo za wenzao kama Khamisi kwa kujikita katika kilimo cha mazao ya matunda na mbogamboga, ufugaji, ufundi stadi, ujasiriamali na miradi mingine ili waweze kujitegemea,” anasema Asha.

Ame Baraka (70), baba yake Khamis anasema alilazimika kumpeleka kijana huyo akiwa amefuatana na wenzake wawili katika Kijiji cha SOS baada ya mama yao mzazi kufariki dunia na kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.

“Wapo watu walinilaumu sana na wengine kunisema kwamba nimewatelekeza watoto wangu kwa kuwapeleka katika vijiji vya watoto... Lakini nilisema sina la kufanya,” anasema.

Mratibu wa Malezi Salama katika Kijiji hicho, Juma Hamadi Shehe, anasema malengo ya Kijiji cha SOS ni kuona vijana wanaopita hapo wanapata mafanikio katika maisha hususani kufanikiwa kujitegemea.

Chanzo: www.habarileo.co.tz